Select Menu

Ads

Random Posts

Powered by Blogger.

Design

Technology

Circle Gallery

Shooting

Racing

News

Bottom

Wednesday, July 23, 2014

Cadaver: Maiti zinazotumiwa na wanafunzi wa sayansi ya tiba

Mwaka 335-280 nchini Ugiriki kabla ya kuzaliwa kwa Kristo alitokea mwanasayansi nchini humo aitwaye Herophilus, huyu ndiye mtu wa kwanza kujenga mafunzo juu ya maumbile ya mwanadamu, kitaalamu ‘Anatomy’.

Mwanasayansi huyu ndiye baba wa somo la Anatomy yaani maumbile ya mwili. Huyu ndiye aliyebainisha kuwa ndani ya mwili wa mwanadamu kuna damu na si hewa.

Kwa kutumia taaluma hiyo alianza kujifunza kufanya upasuaji wa maiti ili kujifunza na kuzifahamu sehemu zinazounda mwili, ikiwamo ngozi, mishipa ya damu, ya fahamu, misuli na ogani za mwilini.

Kutokana na mafanikio yake na umuhimu wake kuelekea katika fani ya tiba, somo la upasuaji wa maiti ulianza kutumika duniani katika vyuo vya tiba.

Ingawa palitokea upinzani wa kidini wakitaka jambo hili lizuiliwe, paliwekwa taratibu maalumu zilizokubalika na kusimamiwa kisheria.

Upasuaji maiti  

Wanafunzi wote wanaosoma sayansi ya tiba duniani mwaka wa kwanza hufanya upasuaji wa maiti ili kujifunza maumbile ya mwanadamu yalivyo, hii husaidia katika fani ya utabibu kwani maiti hizo zinakuwa ndiyo mgonjwa wa kwanza wa mwanachuo.

Mwaka 1831, ilihalalishwa kisheria kwamba miili iliyokosa ndugu au kutotambulika, itumike kwa wanafunzi wa chuo wanaosomea fani ya sayansi ya tiba.
Kwa bahati mbaya hapo baadaye ikaonekana maiti za namna hiyo si rahisi kuzipata huku mahitaji yakiongezeka.

Mwaka 1839 huko Chicago, Marekani ulianzishwa utaratibu maalumu wa kuomba watu kujitolea miili yao pale watakapofariki ili itumike kwa ajili ya kujifunzia maumbile ya mwanadamu. Zikawekwa kanuni na sheria kuhusu muundo mzima wa jambo hilo bila malipo. Taratibu hizo zilirithiwa sehemu mbalimbali duniani lakini hufanyika kwa usiri mkubwa.

Cadaver ni nini?  

Ni maiti za watu ambazo hutumiwa na wanafunzi wa vyuo vya tiba kwa ajili ya wanafunzi kujifunza na kuona maumbile ya mwili mzima.

Maiti hizi zinaweza kuwa ni zile ambazo zimekosa ndugu au kutambuliwa au hakuna anayezitafuta au za watu waliojitolea kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.

Wanafunzi huanza kujifunza kupasua kuanzia kichwani mpaka miguuni. Sehemu ya ngozi ambayo ni ya kwanza huanza kutenganishwa na huchunwa vizuri ili kuwezesha kuona sehemu za ndani za mwili kama mishipa ya damu, fahamu na misuli.
Hii ndiyo sababu ya ngozi ya maiti hizi kukutwa zimechunwa ili kuona vizuri maumbile ya ndani.

Jinsi zinavyotunzwa  

Ikishathibitika kwamba hakuna mtu aliyekwenda kuomba maiti husika kwa kipindi cha miezi 6-12, miili hiyo hukabidhiwa kwa wataalamu wa afya ambao huiwekea dawa maalumu iitwayo 2-phenoxethanol au fomalini.

Dawa hiyo huingizwa katika mshipa mkubwa wa paja na kisha kuieneza sehemu yote ya mwili kupitia mfumo wa mishipa ya damu ili isioze kwa miaka mingi. Hakuna mdudu au mnyama anayeweza kuila au kuigusa, ndiyo maana huendelea kukauka.

Dawa hii ni kemikali zinazoweza kusababisha saratani mwilini kama mtu atakuwa akikumbana nayo kwa muda mrefu na ina harufu kali inayokereketa, pia ni rahisi kuwa kama mvuke ambao mtu akivuta hupata shida kupumua.

Kuhifadhi, matumizi  

Baada ya kuandaliwa, viungo hivi huhifadhiwa katika vyombo au beseni maalumu lililojaa dawa ya maji ya fomalini mpaka pale vitakapohitajika.  Baada ya hapo nchi zilizo mbali hubadilishana maiti hizi. Kwa mfano, Tanzania ambayo iko Afrika Mashariki inaweza kubadilishana na nchi za Afrika Magharibi.
Jambo hili hufanyika kwa umakini mkubwa, haijawahi kuripotiwa mtu aliyekwenda kusoma fani ya tiba akakuta ndugu au rafiki anayemjua akiwa ni cadaver.

Pia katika nchi nyingine, wanafunzi hupewa siku saba kuamua kuendelea na masomo au la, baada ya kutembezwa katika maabara hizi za cadaver na hapa ndipo safari ya kuwa mwanasayansi wa tiba inapoanzia.

Kwa kawaida wanafunzi wanne hutakiwa kutumia cadaver moja na pia hutakiwa kuziheshimu na kutotoa siri za maiti hizo.

Jinsi zinavyotupwa, kuharibiwa  

Maiti hizi baada ya matumizi, mabaki yake huwekwa katika mifuko maalumu na kufungwa vizuri na kurudishwa katika taasisi husika iliyo na mamlaka ya kuzigawa katika vyuo.
Taasisi hiyo ndiyo inayohusika kuzika mabaki hayo.  Baadhi ya nchi huamua kuziteketeza kwa moto na wengine huzizika kama maiti nyingine.

Credit Mwananchi.