Mfanyakazi aliyeteswa. |
“Watuhumiwa wote walikamatwa hivi karibuni na kuhojiwa kisha wakapewa dhamana na upelelezi wetu umekamilika ambapo jalada hilo tumelipeleka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) lakini lilirudishwa polisi kwa sababu kulikuwa na upungufu, akaagiza lifanyiwe kazi tena,” alisema Kamanda Ibrahim.
Aliongeza kuwa baada ya jalada kurudi mikononi mwake alimtafuta mlalamikaji kwa njia ya simu akiwa Mwanza ili aje ahojiwe upya lakini hajaonekana hali iliyofanya alipeleke makao makuu ya jeshi la polisi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
“Ukitaka kupata habari zaidi nenda makao makuu ya polisi jalada la kesi hiyo liko huko,” alisema kamanda huyo. Waandishi wetu walikwenda makao makuu ya jeshi hilo kumuona Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu (pichani), lakini wakaelekezwa kumuona msemaji wake, Advera Senso ambaye alisema upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.
Mlalamikaji wa kesi hiyo ambaye anadai kuteswa na kudhalilishwa aliamua kumwandikia barua ya malalamiko Waziri Mkuu Mizengo Pinda akidai kuwa mwenendo wa kesi yake hauendi vizuri hali iliyomfanya waziri mkuu aliagize jeshi la polisi kulifanyia kazi suala hilo ili haki itendeke.
Waandishi walienda ofisi ya waziri mkuu kutaka kujua kama kuna majibu ya agizo alilolitoa lakini cha kushangaza hakuna majibu yoyote yaliyopelekwa na jeshi la polisi kwa kiongozi huyo kwa mujibu wa maofisa wa ofisi hiyo.
Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu, Irene Bwire alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo, hakuwa na jibu la kuridhisha akaahidi kulifuatilia ili kujua limefikia wapi.
Mlalamikaji huyo anadai kufanyiwa unyama huo Mei 2, mwaka jana na kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Mkoa wa
Kipolisi Kinondoni lakini akadai hakuna kilichofanywa na jeshi hilo badala yake amekuwa akipata vitisho vya mauaji jambo linalomfanya aishi kwa kujificha. Baadhi ya mambo aliyoyalalamikia mlalamikaji ni kupigwa na kujeruhiwa, kudhalilishwa na kudhulumiwa mali zake na mwajiri wake huyo.
Alizitaja baadhi ya mali hizo kuwa ni pamoja na nyumba, magari yake mawili ambayo ni Toyota lenye namba za usajili T 786 BZG na Toyota Fortuner namba T503 BQC, bastola, fedha taslim dola za Kimarekani 100,000, maduka na ofa zake tatu za viwanja huko Kigamboni.
Katika barua aliyompelekea waziri mkuu, mlalamikaji alidai kufanyiwa unyama huo na Awadhi kwa kushirikiana na mabaunsa pamoja na baadhi ya wafanyakazi wake katika chumba maalum wakimtuhumu kuiba dola za Kimarekani milioni 10.