Select Menu

Ads

Random Posts

Powered by Blogger.

Design

Technology

Circle Gallery

Shooting

Racing

News

Bottom

Tuesday, July 15, 2014

Watoto wahamasishwe kushiriki michezo

Mwishoni mwa mwaka jana, uongozi uliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulifanya semina ya mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu au kushiriki katika michezo (grassroot) na baadaye tamasha kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Semina hiyo ilihusisha walimu wa mpira wa miguu kutoka sehemu mbalimbali nchini na tamasha liliwashirikisha watoto zaidi ya 1,500 wa Mkoa wa Dar es Salaam wenye umri kati ya miaka 6-12. 

Semina hiyo ilikuwa muhimu kwa sababu lengo lilikuwa ni walimu waliopata mafunzo, wakafundishe watoto wengi kupenda kushiriki katika michezo au kucheza mpira kwa furaha kwenye shule, mitaani ili kuwa na utamaduni wa Taifa la wapenda michezo kuanzia utotoni. 

Baada ya semina hiyo walimu walipewa vyeti vyenye nembo ya Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) kuonyesha wamehitimu mafunzo hayo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu au kushiriki michezo.

Pia katika tamasha lililofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, watoto walionekana kufurahia tamasha hilo kwani walifundishwa na walimu hao misingi mbalimbali ya soka. Watoto walioneka wakifurahia kukokota mpira, kupokea mpira, kutuliza, kupiga pasi na misingi mingine mingi. 

Sisi tunaamini walimu wale waliohitimu mafunzo hayo wanatumia vyema mafunzo waliyoyapata katika kuhamasisha watoto kushiriki katika michezo na hatutaamini kama walimu hao waliweka vyeti vyao majumbani kwao na kubaki kujisifu tu kwamba wamepata mafunzo ya Fifa. 

Tunaamini uongozi wa TFF uliopo madarakani hivi sasa na wenyewe utafanya semina nyingine ya mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu kwani huo ndiyo mwanzo wa kupata wanamichezo mahiri tangu ngazi ya chini.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia hivi sasa watoto wengi hasa wale wanaotoka katika familia zenye uwezo, wanaathiriwa na kuangalia sana televisheni na kucheza video games hivyo kuwa na wakati mgumu kiafya na kuwa imara kwa sababu hawafanyi michezo inayochangamsha mwili. 

Vile vile wale wanaotoka katika maisha duni wamejikuta wakifanya shughuli za kutafuta kipato ili kusaidia familia zao baada ya masomo badala ya kujishughulisha na michezo.

Tunaamini TFF inajua mtoto akishiriki katika michezo hukua vizuri, hujifunza nidhamu, hujifunza mambo ya msingi ya mchezo huo na hivyo inakuwa rahisi kwake kuendelezwa na zaidi ya yote anakuwa raia mzuri. 

Ikumbukwe kuwa michezo ni furaha, ni burudani, michezo huhusisha akili na mwili, kwa hiyo mtoto anayekua huku akishiriki michezo huusisha akili na mwili kwa kiwango cha juu. 

Tunaushauri viongozi wa vyama vya michezo waige mfano huo kwa kufanya semina za mafunzo ya walimu wa watoto na ikiwezekana kuandaa matamasha kama hayo ambayo hukutanisha watoto kutoka sehemu tofauti na kucheza kulingana na umri wao.

Pia vyama vifanye matamasha katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhamasisha watoto kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuwajengea mapenzi zaidi na michezo na hivyo kuandaliwa vyema kuwa watetezi wazuri wa taifa katika michezo hapo baadaye. 

Cheza mpira wa miguu kama lile lililofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwaka jana kwani yatasaidia kujenga msingi imara wa mchezo huo.