WIKI iliyopita mwigizaji Jennifer Kyaka ‘Odama’ alifafanua mambo mbalimbali aliyopitia maishani likiwemo suala la kuficha ujauzito na mambo mengine ambayo yawezekana ulikuwa huyajui juu yake. Leo tunamalizia makala haya kwa kutazama majibu ya maswali mbalimbali ambayo nilimuuliza na kuyatolea ufafanuzi. UNGANA NAYE…
Mwandishi: Wasanii mnatajwa sana kwenye masuala ya ushirikina ili mng’ae kisanii, kwa nini msimtegemee Mungu?
Odama: Uchawi upo, huwezi kuukwepa lakini inategemea na mtu anaundekeza kiasi gani. Binafsi siamini katika hayo mambo. Namtegemea Mungu zaidi.
Mwandishi: Malengo yenu kama kampuni ni nini katika gemu la filamu za Kibongo?
Odama: Kama kampuni malengo yetu makubwa ni kuvuka mipaka ya Tanzania na kufanya vizuri zaidi ya Wanigeria ambao wanaonekana kututangulia kimaendeleo.
Mwandishi: Kila mtu kwenye sanaa huwa anakuwa na mtu aliyemvutia hadi kuingia, kwa upande wako, ni nani alikufanya uingie kwenye sanaa?
Odama: Msanii ambaye alikuwa akinivutia kabla sijaanza uigizaji ni Monalisa (Yvonne-Chery Ngatwika). Uhalisia wake katika uigizaji ndiyo kitu kilichokuwa kikinivutia kwake ndiyo maana nikaamua kuingia kwenye sanaa.
Mwandishi: Wasanii wengi mnatajwa kuwa mnakwenda nchi za nje kujiuza, hili unalizungumziaje? Odama: Kila mtu ana uhuru wa kusema kile anachojisikia lakini kwa upande wangu sina ‘comment’ (maoni) kwa sababu mimi huwa nikienda nje ya nchi nafuata ishu maalum.
Mwandishi: Ishu maalum ndiyo ipi maana hata wewe uliwahi kutajwa katika sakata hili.
Odama: Weee, uniache kabisa. Mimi mara nyingi nakwenda kwa kazi maalum. Kwa mfano safari yangu ya mwisho kwenda (China) nilifuata vifaa vya ofisi kama kamera na vitu vingine.
Mwandishi: Tunafahamu huna muda mrefu tangu ujifungue, lini sasa utaanza kuingia mzigoni au utabaki kama mkurugenzi na hutaigiza tena?
Odama: Hobi yangu ni kuigiza, siwezi kuacha fani hii kwa sababu naipenda. Nasubiri tu mtoto atimize miezi mitatu, nitaanza kazi kama kawaida. Sasa hivi ana miezi miwili. Mwandishi: Naona umekuwa bongenyanya, huoni kama inaweza kukuharibia ukapoteza mvuto wa kimwonekano utakapoanza kuigiza?
Odama: Ni kweli kwa sasa nimenenepa sana, lakini nafikiria kuanza mazoezi taratibu na nina imani mwili wangu wa kawaida utarudi tu.
Mwandishi: Kwa nini usianze sasa mazoezi, huoni kadiri muda unavyozidi kwenda na wewe unazidi kunenepa?
Odama: Siwezi kuanza mazoezi kwa sasa kwa sababu nilijifungua kwa oparesheni hivyo lazima nikae kama miezi sita hivi ndiyo nipige mazoezi ya nguvu kuepuka kufumua mshono bure.
Mwandishi: Wasanii kwa sasa mna makundi katika mitandao ya kijamii, utakuta timu flani imemdiss flani, hivi unaona kuna umuhimu wowote kwa msanii kuwa na hizo timu?
Odama: Mimi sioni ubaya wa kuwa na hizi timu kwa sababu zinamfanya msanii azungumze kwa ukaribu na mashabiki wake ila tatizo linakuja kwa wale ambao wanazitumia kwa kurushiana matusi, hapo ndipo tatizo linapokuja. Tukizitumia vizuri, hazina madhara.
Mwandishi: Katika maisha yako ya sanaa, ulishawahi kukwazwa na jambo au msanii mwenzako ukateseka kila wakati.
Odama: Huwa napenda kufurahi na kusahau kila wakati, siwezi kukaa na dukuduku moyoni hivyo kama yalitokea nimeshayasahau. Sikumbuki.
Mwandishi: Msanii gani wa kiume anakuvutia jinsi anavyoigiza kwa sasa?
Odama: Walikuwepo wengi huko nyuma ila kama ulivyosema kwa sasa namkubali zaidi Gabo, ni msanii mzuri sana sema kama watu wengi hawajamshtukia.
Mwandishi: Mashabiki wako wangependa kumjua baba wa mtoto huyo na pengine mna mipango gani?
Odama: Mtoto wangu anaitwa Jason kuhusu baba yake watamjua siku si nyingi, wasikonde! Mipango inakuja wakae mkao wa kula.Mwandishi: Asante kwa ushirikiano wako tangu mwanzo hadi mwisho.
Credit GPL.
Saturday, July 19, 2014
Kuhusiana na skendo ya kujiuza mwili, Odama: 'Sikwenda nnje kujiuza'
Labels:
Entertainment,
Gossip,
Life Style