Select Menu

Ads

Random Posts

Powered by Blogger.

Design

Technology

Circle Gallery

Shooting

Racing

News

Bottom

Showing posts with label Future. Show all posts
Showing posts with label Future. Show all posts

Tuesday, August 5, 2014

Bibi ajitengenezea jeneza baada ya kuchoshwa na dhiki

Kila siku naomba Mwenyezi Mungu anichukue haraka ili nikapumzike kutokana na mateso ninayoyapata, lakini hofu yangu nikifa je, nitazikwa kama binadamu wengine? Ndiyo maana nimeamua kujitayarishia jeneza langu,” anasema Scholastica Mhagama (76) mwenye ulemavu wa viungo anayeishi pekee yake katika kibanda kilichoezekwa kwa nyasi. 

Bibi huyo mkazi wa Kijiji cha Lundusi Kata ya Peramiho wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, anasema kwa miaka mingi ameishi katika kibanda hicho alichojengewa na mzungu aliyemtaja kwa jina moja la Kilibada ambaye pia anasema alikuwa akimsaidia kulima mihogo. 

Anaongeza kuwa maisha yake yanategemea kukaa nje ya kibanda chake na kuomba msaada kwa watoto wanaopita ambao huwaomba wamchotee maji. 
Bibi Scholastica akiwa ameegemea jeneza lake.
 
Anabainisha kuwa mara chache anaweza kutokea mtoto ambaye humchotea maji kwenye ndoo ndogo ya lita kumi ambayo huyatumia kwa matumizi ya kuoga, kupikia, kunywa na kwamba hayatoshi kufulia wala kufanya kazi nyingine hali ambayo inamsababishia kuvaa nguo chafu wakati wote.

Anasimulia kuwa huwa anapika mara chache ndani ya kibanda anacholala na hata sehemu anayolala haina kitanda, godoro wala mkeka badala yake amekuwa analala chini katika mfuko wa mbolea na kujifunika blanketi kuu kuu. 

Ona kwanza mwanangu mahali ninapolala hakuna kitanda wala mkeka, mifuko ambayo ndiyo godoro langu huwa ninaomba tu. Nahitaji msaada, sina uwezo wa kufanya kazi yoyote tangu nilipokatwa mguu wa kulia nilipokuwa darasa la tatu hadi sasa nimekuwa naishi kwa shida ingawa sasa katika uzee hali imekuwa mbaya zaidi,’’ anasema. 

Ajitengenezea jeneza  

Kutokana na kushindwa kupata msaada kutoka kwa ndugu na majirani zake, Scholastica ameamua kutengeneza jeneza lake kabla ya kufa akihofia kuzikwa katika mkeka kwa kuwa ameshindwa kusaidiwa akiwa hai, hivyo anaamini akifa anaweza kutupwa kama mzoga wa mnyama asiye na faida yoyote.

Nimetengeneza kabisa jeneza langu siku nikifa wanizike humu. Naomba Mungu anichukue haraka ili kuepukana na mateso haya. Nimetengwa na jamii na majirani wanashindwa kunisaidia wanadai eti mimi ni mchawi kwa sababu watoto wangu wote wanne walikufa wakiwa wadogo. Naumia sana kusingiziwa kitu ambacho sikijui,’’ anasema kwa masikitiko. 

Bibi huyo anasema kuwa aliweza kutengeza jeneza hilo baada ya kupewa Sh40,000 na mfadhili mmoja. 

Tayari nilikuwa na mbao kwangu, hivyo kazi ilikuwa kumlipa kijana fedha na kumpa mbao ili anitengenezee jeneza,” anasema. 
Hata hivyo, aliitaja misaada ya haraka ambayo anahitaji ili aweze kuishi kuwa ni pamoja na baiskeli ya miguu mitatu (wheel chair) ambayo itamwezesha kutembea kwa kuwa hivi sasa amekuwa anatambaa na kupata maumivu makali kutokana na nyama iliyobakia kwenye nyonga baada ya kukatwa mguu.

Pia bibi huyo anahitaji msaada wa bati kwa ajili ya kuezeka kibanda chake kwa kuwa wakati wa masika mvua humnyeshea na kupata mateso makubwa. 

“Mvua yote inaishia mwilini mwangu. Huwa naugua na kupata homa kali lakini Mwenyezi Mungu bado hataki kunichukua. Napata vichomi kutokana na baridi kali hasa usiku hadi inanilazimu kuwasha moto kila siku usiku walau kupata joto. 
Kwa kweli natamani kufa lakini Mungu bado hajasikia kilio changu anataka niishi,’’ alisema kwa masikitiko. 

Alidai kuwa kuna watu walifika kumuandikisha jina na kumuingiza katika orodha ya watu wanaostahili kupata msaada na kwamba amekuwa anasikia misaada inafika kwa jina lake, lakini hajawahi kupewa hata shilingi.

Hajanywa chai kwa miaka 15  Akisimulia dhiki kuu aliyonayo bibi huyo anasema kwa siku walau anapata milo miwili, lakini chai hajawahi kunywa kwa miaka 15 sasa na kwamba kila siku anakula ugali kwa mboga ya majani aina ya ‘Chinese’ ambayo amekuwa anaomba na kupewa na wasamaria wema wanapopita njiani na kwamba katika kipindi cha miaka kumi sasa hajawahi kula nyama wala samaki. 

Anasema kulingana na matatizo aliyonayo ilitakiwa apelekwe katika kituo cha kulelea wazee wasiojiweza. Hata hivyo, Idara ya Ustawi wa Jamii imeshindwa kumsaidia kwa madai kuwa bibi huyo anaye kaka yake ambaye anamuelezea kuwa ni mzee asiye na uwezo wa kumlea. 

“Mwaka jana mwezi wa 10 nimelima hapa uwanjani matuta 12 kwa kushika jembe huku nimekaa chini na kujivuta, waulizeni majirani watawaambia ninahitaji msaada sina nguo, maji, sabuni, mafuta, pesa za matumizi mimi maisha yangu ni ya kuombaomba tu, alisema. 

Katika enzi za ujana wake wake Scholastica anasema alibarikiwa kupata watoto wanne ambayo wote walifariki wakiwa wadogo.

Hata hivyo kaka yake aitwaye Joackim Mhagama amekiri kuwa mwanzoni alipokuwa ana nguvu alijitahidi kumsaidia, lakini kutokana na umri kwenda ameshindwa kwani naye anahitaji msaada. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lundusi chenye wakazi zaidi ya 2,500, Kelvin Mahundi amekiri kutambua matatizo aliyonayo Scholastica Mhagama na kwamba walimpeleka ustawi wa jamii ili kuhakikisha anapelekwa katika kituo cha serikali cha kulelea watu wasiojiweza. 

Anasema bibi huyo ilishauriwa apelekwe katika kituo cha Ngei wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma. Hata hivyo, hafahamu sababu zilizosababisha hadi sasa kutopelekwa katika kituo hicho ili aweze kusaidia hadi mwisho wa maisha yake.

Anasema hadi sasa kijiji hakina fungu la kusaidia watu wasiojiweza ingawa yeye kama mwenyekiti alipeleka taarifa zake kwa watu kama Abasia ya Peramiho ambao awali walikuwa wanatoa msaada pamoja na chama cha wenye ulemavu na kwamba inawezekana umri wake na ulemavu wake vinasababisha kushindwa kupata huduma muhimu. 

Kutokana na hali zao wanawake wazee wenye ulemavu kama ilivyo kwa Scholastica wanaishi katika maisha duni na ushiriki wao katika kazi za jamii ni mdogo kutokana na kukosa fursa na nyenzo za kuwasaidia kuleta maendeleo. 

Sera ya wazee  

Sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 inabainisha kuwa suala la uzee na kuzeeka limekuwa lenye umuhimu mkubwa ambapo karne ya ishirini imeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wazee.

Kulingana na takwimu zilizopo, Tanzania inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 itaongezeka na kufikia milioni 8.3 (asilimia 10 ya watu wote). 

Hata hivyo, mwaka 2050, idadi ya wazee, kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu, inatarajia kuongezeka na kuzidi ile ya watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 24. Idadi hiyo katika Bara la Afrika pekee inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 38 ya sasa na kufikia milioni 51. 

Taarifa za Umoja wa Mataifa ya mwaka 1999 inaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya wazee duniani na kwamba ongezeko hilo linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko havilingani na uwezo wa rasilimali zilizopo za kuwahudumia wazee. 
Katika nyanja za afya, lishe na huduma nyingine za msingi kwa maisha ya binadamu.

Credit Mwananchi.

Sunday, August 3, 2014

Fahamu kuhusiana na Magonjwa ya uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke

Kwa wanawake tatizo lao kubwa ni ‘Fibroid’ ambao ni uvimbe katika sehemu za uzazi (uterus) ambapo hutengenezwa na kambakamba zilizofungamana yaani muscle fibre. Fibroid huanza kwa ukubwa kama punje ya njugu mawe lakini huweza kukua na kuwa kama boga. 

Fibroid hupatikana zaidi kwa wanawake wa umri kati ya miaka 30 na 40 na hupungua ukubwa mara tu wanapoingia katika umri wa utu uzima, ingawa sababu au chanzo hasa cha fibroid hakijulikani, utafiti unaonyesha kuwa huchochewa na ‘oestrogen’ mwilini. 

Mara nyingi fibroid hukua kwa mwanamke pale kiwango cha ‘oestrogen’ kinapoongezeka mwilini na pia fibroid hupungua wakati kiwango cha ‘oestrogen’ nacho kikipungua.

Oestrogen ni mkusanyiko wa homoni ambazo ndizo zinazoukuza mwili wa mwanamke kijinsia. Mfano ni ukuaji wa viungo kama matiti na kupata hedhi. 

Pia wanawake wenye uzito wa zaidi ya kilo 70 wana hatari kubwa zaidi ya kupata tatizo hili kutokana na kiwango kikubwa cha oestrogen katika umri huo.Zamani fibroid ingeweza kusababishwa na matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango kwa sababu vidonge hivyo vilikuwa na kiwango kikubwa cha oestrogen. Hivi sasa vidonge hivi havina kiwango kikubwa cha oestrogen kama ilivyokuwa zamani. 

Fibroid zinatofautishwa kutokana na sehemu ilipotokea. Zipo zinazotokea ndani ya mji wa mimba na nyingine zinatokea kwenye kuta za nje ya mji wa mimba. Karibu asilimia 75 ya wanawake wenye fibroid hawajui kama wana tatizo hilo. Utambuzi wa dalili za fibroid hutegemea ukubwa wake na wapi zilipo kwenye kizazi. Hii pia huchangiwa na dalili anazopata mtu.Fibroid ndogo iliyo kwenye kuta za kizazi haitakuwa na dalili sawa na fibroid kubwa inayoota nje ya kizazi.

DALILI 

Dalili kubwa inayofahamika zaidi ni ile ya kutokwa damu nyingi wakati wa hedhi na  maumivu ya tumbo.
Pia huathiri mfumo wa haja ndogo na kubwa, na mgonjwa kuhisi mkojo mara kwa mara, mkojo kutoka kidogokidogo, kushindwa kutoka kirahisi, kukosa choo, kutopata mimba na kupata maumivu wakati wa tendo la ndoa. 

Fibroid zaweza kusababisha matatizo kama kuharibu mimba au mwanamke kutoshika mimba kutokana na mirija ya uzazi kubanwa au msukumo unaosababishwa na fibroid, mirija ya uzazi hubanwa na hivyo kushindwa kupitisha mayai kuelekea kwenye kizazi (uterus). 

Mwanamke anapokuwa mjamzito pia akawa na fibroid, mwili huweza kusitisha kupeleka damu kwenye fibroid na kuifanya isinyae hivyo kusababisha maumivu makali ya tumbo na kufanya kizazi kutanuka na kusinyaa na baadaye mimba huweza kutoka kabla ya wakati wake. 

Wakati wa kujifungua, kama fibroid itakuwa kwenye njia ya kutolea mtoto inaweza kusababisha damu nyingi kutoka au ikishindikana, mama hufanyiwa upasuaji ili kumtoa mtoto aliye tumboni.

USHAURI  

Dalili zikiwepo na kuhisi unalo tatizo la fibroid, mwone daktari kwa ajili ya kupata vipimo kujua kama unao ugonjwa au la. Daktari atafanya vipimo vya ‘Ultrasound’ (mionzi) au kitatumika kifaa kidogo ambacho huingizwa kwenye kizazi kupitia sehemu ya uke kitaalamu huitwa hysteroscopy au kufanyiwa upasuaji wa sehemu ndogo ya tumbo pamoja na kuwekewa kifaa kidogo sehemu ya uke kitaalamu huitwa Laparosopy.

TIBA   

Kuna njia kuu mbili za kutibu fibroid. Moja ni kwa kutumia dawa. Mkusanyiko wa dawa zijulikanazo kama ‘GnRH analogues’ hupunguza kiwango cha oestrogen mwilini na hivyo kusababisha fibroid kusinyaa.
Dawa hizi zikitumika kwa miezi sita hupunguza ukubwa wa fibroid pia hupunguza mzunguko wa hedhi.

Matumizi ya dawa za ‘GnRH analogues’ yasizidi miezi sita kwani dawa hizi huweza kuleta madhara makubwa baadaye.
Mara baada ya kuacha kutumia dawa hizi,wanawake wengine baada ya wiki chache hujikuta wakirudiwa na tatizo hili ambalo huanza kukua tena na mwanamke huanza kupata hedhi kama awali lakini ikiambatana na maumivu makali.
Baadhi ya wanawake huwa hawapati hedhi tena kwa maisha yao yote. 

Upasuaji ni njia nyingine ya kutibu ugobnjwa huu na huhusisha mambo yafuatayo: Kuiondoa fibroid yenyewe na kuacha kizazi jambo ambalo kitaalamu huitwa myomectomy; kukiondoa kizazi kabisa kitaalamu huitwa hysterectomy na kuzuia damu kwenda kwenye fibroids  yaani uterine artery embolisation. 

Pia iko njia ambayo mtu huchomwa sindano nne tumboni kwa ajili ya kuziua kwa kemikali maalumu.

Credit GPL.

Video: Kutana na mzee huyu anayefuga Mamba nyumbani kwake

Kutana na mzee huyu anayefuga Mamba nyumbani kwake katika mtaa wa Gatumba mjini Bujumbura Burundi.
Nini hasa kilichompelekea kuanz kufuga wanyama hawa hatari nyumbani kwake?


Saturday, August 2, 2014

AFYA YA UZAZI: Tatizo la kutopata ujauzito

Mtu anaposema tatizo la kutopata ujauzito, ana maana mume na mke walio katika uhusiano wa kutafuta mtoto ndani ya mwaka mmoja, lakini wameshindwa. 
Inaweza ikawa zaidi ya mwaka mmoja lakini wastani wa kiwango cha chini ni mwaka mmoja. 

Ni tatizo kubwa katika jamii kwani kila mmoja anataka afikie malengo ya kuwa na familia. 
Mwanamke na mwanamume wote wanahusika katika tatizo hili japo mara nyingi huonekana ni la mwanamke. Kutoshika mimba kwa muda mrefu ni ugumba ua infertility kwa kitaalamu. Mwanamke au mwanaume anaweza kuwa mgumba.

Ugumba umegawanyika katika maeneo makuu mawili. Kwanza ni ‘primary infertility’ ambapo mwanamke hana historia ya kuwa na mimba wala mwanaume hana historia ya kumpa mwanamke mimba. 

Ugumba wa aina ya pili ni ‘secondary infertility’ ambapo mwanamke anayo historia ya kuwahi kupata ujauzito, haijalishi kama alizaaa au mimba ilitoka na mwanamume anayo historia ya kumpa mwanamke mimba na pia haijalishi kama mtoto alizaliwa au mimba ilitoka. 

Tatizo la mwanamume kutoweza kumpa mwanamke mimba linaweza kusababishwa na kukosa nguvu za kiume hivyo kushindwa kufanya tendo la ndoa.

Hali hii ya kukosa nguvu inaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali kwani yenyewe si ugonjwa.  Kwa hiyo kitu cha msingi siyo kuongeza nguvu bali ni kufanya uchunguzi kuona tatizo ni nini na kulipatia ufumbuzi. 
Tatizo lingine kwa mwanamume ni kutotoa mbegu za kiume za kutosha ua kutoa mbegu zisizo na ubora. 

Hii ni baada ya kupima kipimo cha mbegu za kiume. Mbegu zinaweza zisizalishwe ua zikazalishwa pasipo na ubora unaostahili kurutubisha yai la mwanamke. 

Matatizo mbalimbali yanaweza kuathiri uzalishaji wa mbegu za kiume kama uvutaji wa sigara,  unywaji wa pombe kali, maumivu ya korodani na utumiaji wa dawa za kulevya kama mirungi na bangi.

Mazingira ya joto katika korodani pia huathiri uzalishaji wa mbegu. Kutofahamu mzunguko wa hedhi wa mwanamke na kipindi gani mwanaume anaweza kumpa mimba ni changamoto nyingine kwa upande wa mwanaume. 

Itaendelea wiki ijayo...

Credit Mwanancvhi.

Friday, August 1, 2014

AFYA YA NGOZI: Maradhi ya ngozi kwa njia ya ngono

Baadhi ya maswali tuliyopokea, mengi yalihusu maradhi ya sunzua ambayo kitaalmu yanajulikana kama warts.  
Sunzua ni ugonjwa wa ngozi unaofahamika na wengi. Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo kitaalamu huitwa human papilloma virus. 

Karibu asilimia 10 ya wanadamu wamewahi kupata athari za virusi vya ugonjwa huu, achilia mbali kuumwa sunzua. 
Kwa sababu hiyo ndiyo kusema kila mtu anapaswa kufahamu ugonjwa huu kwa undani ili unapojitokeza awahi hospitali ili kuudhibiti.

Virusi vinavyosababisha ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya ngono. 
Ugonjwa huu hutokea sehemu mbalimbali za mwili, lakini huwatokea wengi sehemu za siri. 
Sunzua kama ugonjwa wa zinaa, huathiri sehemu za siri pamoja na njia ya haja kubwa. 

Wagonjwa ambao wanaishi na Virusi vya Ukimwi wako kwenye mazingira hatarishi zaidi ya kupata sunzua.   
Virusi vinavyosababisha maradhi ya sunzua huambukizwa kwa njia ya ngono na ni mara chache huweza kusambaa kwa njia ya kugusana.

Virusi wa maradhi haya wanajulikana kama papilloma na hujitokeza kwenye eneo la ngozi ambapo virusi hivi vimepenya. Mara nyingi hujipachika kwenye mchubuko au mpasuko wa ngozi. 
Maradhi haya huweza kujitokeza kwenye ngozi kati ya miezi miwili hadi tisa baada ya kupenya kwenye ngozi. 
Maradhi haya husababisha ngozi kutokuwa na muonekano wake wa kawaida.

Husababisha ngozi kuwa na milima na mabonde kiasi cha kusababisha kukatika kwa urahisi na kufanya virusi kuendelea kupenya. 
Dalili za maradhi haya ni kuwa na ngozi iliyoinuka, iliyopoteza unyoofu wake na yenye muonekano mfano wa maua. 

Sunzua ziko za aina tofauti kulingana na mahali ugonjwa unatokea na kuonekana kuiathiri ngozi. 
Sunzua ya sehemu za siri au kwa kitaalamu condyloma acuminatum (venereal warts).

Aina hii ya ugonjwa kwa wanawake huathiri sehemu za nje za maumbile ya siri na mara nyingine huweza kujitokeza na kuathiri shingo ya kizazi. 
Kwa wanaume sunzua huathiri uume wenyewe, korodani, nyonga mpaka kwenye mapaja. 

Sunzua hii ya sehemu za siri kwa watu wa jinsia zote hujitokeza kama uvimbe ulioinuka au zikawa sawia bila uvimbe wa aina yoyote. 
Sunzua zinaweza kuwa kubwa au ndogo, zikawa mojamoja au zikajikusanya pamoja kama mafungu zikafanana kabisa na maua.

Huwa zinaweza kutokea usoni, hasa sehemu karibu na kope ama maeneo mengine kama vile vidole vya miguu na mikono. 
Sunzua huwa haziumi na sanasana huwa zinawasha na huweza kujitokeza katika kipindi cha miezi miwili mpaka tisa baada ya maambukizi ya virusi. 

Kwa wanawake, sunzua ya kwenye shingo ya kizazi huweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi. 
Kwa sababu hiyo, mwanamke anapaswa kujichunguza ili kuchukua hatua mwafaka za matibabu.

Ndugu msomaji, kwa jumla magonjwa ya ngozi ni mengi na yanaathiri binadamu kwa namna tofauti. Kama nilivyoeleza hapo awali, yanayotokana na bakteria, fangasi, virusi na hitilafu nyingine katika damu au ngozi. 
Tutaendelea kujibu maswali mbalimbali ya wasomaji kulingana na mtakavyouliza. Kwa wale ambao maswali hayakujibiwa wasikate tamaa kwani kadri tutakavyopata nafasi, yataendelea kujibiwa.

Mawasiliano: isaac.I.Maro@gmail.com  

Credit Mwananchi.

Thursday, July 31, 2014

Video: Gari hili linaweza kutumika miaka 100 bila kuongezwa mafuta

Moja kati ya mambo ambayo mtu wa anayafikiria kabla hajanunua gari ni kiasi cha mafuta kinachotumiwa na gari hilo. Lakini ukiwa na gari hili… unaweza usifikirie kabisa kuhusu mafuta huku ukilitumia kama kawaida kwa zaidi ya miaka 100.

Wataalam wa masuala ya magari wameeleza kuwa endapo gari linalotumia ‘Thorium’ litaanza kufanya kazi litakuwa gari ambalo linaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 100 bila kuongezwa mafuta.

Kwa maana hiyo Thorium itakuwa na uwezo wa kudumu hata zaidi ya maisha ya mtumiaji wa gari hilo.

Kampuni ya Laser Power tayari imeshatengeneza idea ya kutumia Thorium katika engine za magari  ambapo wataitumia kitaalam kuchemsha maji na kuwa chanzo cha nguvu ya kuendesha gari.

Hata hivyo, CEO wa Laser Power System, Dr. Charles Sevens aliiambia Mashable kuwa engine za Thorium hazitaweza kuwa kwenye magari hivi karibu kwa kuwa watengenezaji wa magari hawataki kuzinunua.

Cars are not our primary interest. The automakers don’t want to buy them.” Alisema Dr Charles Stevens.

Alisema makampuni mengi ya magari yanataka kutengeneza pesa zaidi kwa kutumia engines za gas na kwamba itawachukua miongo kadhaa kukubali na kuanza kutmia teknolojia ya Thorium.

Endapo gari hili litafanikiwa kuingia sokoni na kununuliwa na watu wengi miaka ijayo, itakuwa hatari kwa biashara ya mafuta hasa kwa wale wanaotegemea magari pekee kufanya mauzo.

Friday, July 25, 2014

Hizi hapa ndizo Sababu 10 zinazotia moyo dawa mpya ya Ukimwi

Wiki hii imekuwa na habari njema na ya faraja kwa dunia katika kupambana na Virusi Vya Ukimwi (VVU). 

Wengi wanaweza kujiuliza mbona mambo ya ugunduzi wenye kutia matumaini yamewahi kutangazwa siku za nyuma, lakini yakaangukia pua? Kwa nini hata huu wa sasa usifuate mkondo huo? 

Haya ni mambo ya kisayansi ambayo yanaaminika kila hatua inayopigwa inamsogeza mtafiti kwenye kupata jawabu hata kama hakufaulu. 

Wanachofanya wanasayansi ni kutumia udhaifu uliojitokeza katika tafiti moja kuwa ni faida ya kumfanya afanye vizuri katika nyingine atakayofanya. 

Utafiti uliotangazwa wiki hii umeonekana kutegua kitendawili ambacho kilionekana kuwatatiza wanasayansi wengi.

Huu ni utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple nchini Marekani kilichopo katika mji wa Philadelphia. 

Wao wamegundua tiba ya kuangamiza VVU ambayo wanaielezea kuwa ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na tafiti nyingine zilizowahi kufanyika duniani. 

Dawa hii inaweza kutumika kama tiba kwa wale ambao wanaishi na VVU pamoja na kuwa kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa. 

Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili anasema wao wamegundua namna ya kuweza kukiondoa kirusi cha Ukimwi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua. 

Anasema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuiathiri seli ya mwili wa binadamu iliyoingiliwa na kirusi.

Dk Khalili anasema kuwa ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia nyingine ambazo tayari zimegunduliwa zimekuwa haziwezi kupenya ndani ya seli ya binadamu bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake; ndani ya mfumo wa damu. “Dawa zilizopo haziwezi kukiathiri kirusi cha Ukimwi kilichopo ndani ya seli, bali kile ambacho kimezalishwa na kuingia kwenye mfumo wa damu tayari kwenda kushambulia seli (CD4) nyingine,” anasema Dk Khalili. 

Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo ARV (dawa ya kufubaza VVU).”

Kwa namna ARV zinavyofanya kazi, huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kushindwa kuvikabili vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4 hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi muathirika akiacha kutumia dawa. 

Kutokana na maelezo ya Dk Khalili, dawa hiyo ina sifa 10 muhimu ambazo zinadhihirisha kuwa ni ya matumaini. 

Sifa hizo ni dawa kuweza kugundua seli iliyoingiliwa na kirusi, kutoboa seli kwa usalama na kuvuta nje ya seli kirusi kwa kuking’oa kwenye DNA. 

Dawa hiyo huiacha DNA; sehemu iliyong’olewa ikijitengeneza huku seli nayo ikijitengeneza palipobomoka. Kirusi kufa baada ya kutoka nje ya seli, seli iliyoondolewa kirusi hubaki salama na kuendelea na kazi ya kinga kama kawaida.

Sababu nyingine ni dawa kuweza kufanya kazi pamoja na ARV na vilevile ugunduzi huu umeweza kutegua kitendawili kilichowatatiza wanasayansi wengi cha kuweza kushambulia kirusi ndani ya seli bila kuiathiri. 

Mpaka sasa dawa nyingi zilizogunduliwa zinapambana na virusi walioko nje ya CD4. Jambo jingine muhimu ni dawa hiyo mpya kuweza kufanya kazi vizuri kwenye damu ya binadamu bila dalili za kuathiri seli nyingine.  Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa

Magonjwa ya Binadamu, Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani anaelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU. “Kama imepatikana teknolojia ya kuweza kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili limeonekana kuwa gumu kwa muda mrefu,” anasema Majani.

Anasema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo limekuwa gumu. 

Maana inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo ki tiba halikubaliki,” alisema Majani. 

Kikubwa katika ugunduzi huo ni kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa; ikiwepo ARV,” alisema. 
Hata hivyo, Majani anasema changamoto ambayo inaweza kujitokeza ni ya majaribio ya usalama wa dawa wakati wa matumizi. 

Lazima ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na utendaji wa mwili kwa jumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi zinashindwa… Tusubiri tuone labda hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” anasema Majani.


Uwezo wa dawa  

Dk Khalili anasema wameitengeneza kwa protini maalumu ambayo inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta nje. 
Baada ya kukivuta nje kirusi, huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga ya mwilini kama kawaida. 

VVU kwa kawaida wanashambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama koloni la kuzalishia virusi wengine. 

Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kiumakini na bila kuathiri seli,” anajigamba Dk Khalili.

Anasema tayari dawa yao imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama. Katika maabara, anasema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100. 

Anasema anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache lakini anaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu. 
Dk Khalili alisema wanachofanya kwa sasa ni kuangalia mfumo bora ambao utatumika katika kutibu binadamu.


Mkutano wa Ukimwi 2014  

Ugunduzi huo umekuja wakati ambapo wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli ambazo hazina matumaini ya asilimia 100 ya kupatikana tuba au chanjo, ukilinganisha na mkutano wa mwaka uliopita. 

Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za tafiti za VVU waliweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio.

Tafiti nyingi zikiwa ni za chanjo pamoja na tiba zimeshindwa kupata suluhisho la kudumu kwa sababu dawa zake zinapotumika vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya. 

Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili visiathirike kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” anasema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty nchini Australia, Professor Sharon Lewin. 

Hata hivyo, Mwenyekiti wa mkutano huo wa Ukimwi 2014, Profesa Françoise Barré-Sinoussi anasema ARV imewezesha kubadili kasi ya VVU na kinachoonekana sasa ni kiwango cha maambukizi kinapungua kadri miaka inavyoenda.

Profesa Barré-Sinoussi anasema: “Hatuna budi kusema programu hii ya kukabili imefanya mambo makubwa katika kukabiliana na janga hili na kubadili mwelekeo.” 

Anasema takwimu zinaonyesha kuwa karibu waathirika 14 milioni ambao ni wa kipato cha chini na cha wastani, wanatumia ARV, hali ambayo imesaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa VVU. 

Pamoja na hali hiyo, Profesa Barré-Sinoussi anasema kazi iliyopo mbele kwa sasa ni kupata tiba na chanjo na kwamba anaamini mafanikio yatapatikana.

Hali ya Ukimwi duniani  

Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty nchini Australia, Professor Sharon Lewin anasema tafiti za sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 34 duniani wanaishi na VVU.

Anasema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambapo bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika. 
Profesa Lewin anasema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, wanasayansi wamepiga hatua kubwa katika kudhibiti VVU. 

Anasema anaamini juhudi za kisayansi zitawezesha dunia ifikie mahali ithubutu kusema “HIV havina nafasi katika mwili wa binadamu.”  Kwa sababu hiyo, anaamini ipo siku mafaniko yatapatikana kwa kupata chanjo na tiba. 

Ukimwi ulianza kuisumbua dunia miaka 30 iliyopita ambapo miaka ya 1980 ulisababisha vifo vya mamilioni ya watu huku kukiwa hakuna aina yoyote ya tiba.

Mwishoni mwa miaka ya 90 zilianza kutumika ARV ambazo zimesaidia waathirika wengi wasifikia hatua ya kuugua Ukimwi.  Awali waathirika waliofikia hatua ya kuugua Ukimwi walionyesha kuishiwa nguvu, kudhoofika kiafya, nywele kunyonyoka, kupata vidonda sehemu mbalimbali za mwili na kuharisha.

 Kauli ya wanasayansi kwenye mkutano huo ni kwamba “mwathirika wa VVU ametoka hatua ya kuhesabu ni ugonjwa unaomhukumu kufa hadi kufikia kwenye faraja ya kudhibiti virusi ili aendelee kuishi.” 
VVU inaaminika ni kirusi aliyetoka katika jamii ya nyani akajibadili kitabia akaweza kumtumia binadamu kama sehemu ya kumuwezesha aishi na kuzaliana.

Credit Mwananchi.

Kaswende, mawazo, vyaweza kukusababishia uwe na kipara

Kipara ni kitu ambacho kinawapata watu wengi walioko sehemu mbalimbali duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia 50 ya wanaume kwa nyakati tofauti maishani mwao hujikuta wanapata kipara. 
Siyo wote wenye vipara mitaani vinatokana na uasilia. wengine ni kutokana na magonjwa na wengine ni mawazo

Kwa wanaume, mara chache kipara, kinaweza kuanza mapema kati ya umri wa miaka 14 na 20, lakini wanaume walio wengi hupata kati ya umri wa miaka 30 na 60. 

Wanaume wanaopata kipara huanza kuona nywele zikipungua kichwani hatua kwa hatua, kuanzia upande wa mbele au katikati ya kichwa na hatimaye sehemu hiyo huwa haina nywele kabisa.

Ingawa kimsingi kipara hufikiriwa kuwa ni tatizo la kawaida kwa wanaume, wanawake pia wanaweza kukabiliwa na tatizo hili.

Inasemekana kuwa karibu asilimia 40 ya wanawake nchini Marekani, kutokana na sababu mbalimbali wana tatizo la kipara au kunyonyoka nywele kichwani.  Kila unywele huota na kukua katika kifuko cha nywele kiitwacho kinyweleo kilichoko kwenye ngozi. 

Chini ya kila kinyweleo kuna kituta ambacho hushikilia unywele na kituta hiki hujulikana kama foliko ya nywele. 

Katika hali ya kawaida wastani wa nywele 50 hadi 100 huchomoka kila siku kutoka katika vifuko vyake katika ngozi ya kichwani na kuanguka chini.

Jambo hili linaweza kugunduliwa kwa urahisi kwa kuona nywele kwenye vitana, chanuo au foronya tunazotumia wakati wa kulala. 

Nywele zinapochomoka kwa wingi kuliko kawaida kila siku au zisipoota na kukua ili kuziba pengo la nywele zilizotoka, baada ya muda mtu huwa na kipara. Wakati mwingine nywele hupungua bila kutoka kichwani. 

Hali hii inaweza kusababishwa na kupungua kwa unene wa unywele au kutofautiana kwa kasi ya kukua kwa nywele. 
Ingawa chanzo hasa cha upara hakifahamiki vizuri, wanasayansi wanasema kuwa kukosekana kwa usawaziko sawia wa homoni ya kiume ya androjeni aina ya dihydrotestosterone (DHT) mwilini, ni moja ya vyanzo vya tatizo hili. 

Homoni hii inapoongezeka mwilini hasa katika ngozi ya kichwa, husababisha mgandamizo wa ngozi ya katikati ya kichwa na kuathiri foliko za nywele kwa kuzifanya ndogo kiasi kwamba zinapoteza taratibu uwezo wake wa kutokeza nywele mpya.

Hii ni kwa mujibu wa Dk Emin Tuncay Ustuner, daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha sura katika Jiji la Ankara nchini Uturuki. 

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa kutokea kwa kipara kuna uhusiano wa karibu na urithi wa vinasaba au viasili vya kijenetiki vinavyoathiri kuota na kukua kwa nywele katika kipindi fulani. 

Utafiti uliofanyika nchini Japan na kuongozwa na Profesa Yumiko Saga wa taasisi ya taifa ya vinasaba katika Jiji la Mishima, ulibaini kuwa viasili vya kijenetiki aina ya Sox21 vinahusika kwa namna moja ama nyingine na utokeaji wa kipara.

Utafiti mwingine, uliofanywa na timu ya watafiti waliokuwa chini ya uongozi wa Dk Krzysztof Kobielak, unahusisha viasili vya kijenetiki aina ya Wnt na BMP (Bone Morphogenetic Protein) na kutokea kwa kipara. 

Utafiti huo ulibaini kuwa protini aina ya Wnt inapopungua na BMP inapoongezeka, husababisha seli zinazozalisha foliko za nywele kushindwa kufanya kazi na nywele hushindwa kuota au kukua. 

Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika jarida la kisayansi la Stem Cells, la Septemba na Novemba 2013. 

Katika utafiti wao, Dk Lin-hui Su na Tony Hsiu-His Chen uliochapishwa katika jarida la Archives of Dermatology, toleo la 143 la Novemba 2007, walibaini kuwa sumu zinazopatikana katika moshi wa tumbaku pia zinaweza kuathiri foliko za nywele na kuharibu usawaziko wa homoni za kiume mwilini.

Jambo ambalo huchangia kutokea kwa tatizo la nywele kushindwa kuota na kukuwa vizuri hasa kwa wanaume wenye homoni nyingi. 

Matatizo mengine ya kiafya yanayohusishwa na kutokea kwa kipara ni tatizo la muda mrefu la msongo mkali wa mawazo, ugonjwa wa kaswende, tiba ya mionzi, matumizi ya dawa za kutibu saratani na matumizi ya dawa zenye homoni. 
Matatizo mengine ni pamoja na lishe duni kwa muda mrefu, ugonjwa wa tezi la shingo pamoja na matumizi yaliyokithiri ya dawa za kulainisha nywele zenye kemikali kali. 

Ingawa kipara hakiwezi kusababisha mtu apoteze maisha, kinaweza kuwa na athari za kisaikolojia kwa watu wengi hasa vijana wanaopenda mitindo mbalimbali ya urembo wa nywele. 
Jambo hili katika nchi zilizoendelea huwafanya baadhi ya watu kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha kipara.

Hapa kwetu Tanzania, hospitali za rufaa zinao madaktari wa magonjwa ya ngozi wanaoweza kutoa msaada na ushauri kuhusu namna bora ya kukabiliana na tatizo la kunyonyoka kwa nywele au kipara. 

Ili kukabiliana na athari za kisaikolojia zitokanazo na kipara hasa pale inapokuwa vigumu kupata fursa ya kumwona daktari, mtu mwenye tatizo hili anaweza kuvaa wigi au kunyoa nywele zote mara kwa mara. 

Kwa ajili ya kukinga ngozi ya kichwa isiathirike kwa mionzi ya jua, mwenye kipara anaweza kuvaa kofia hasa wakati wa jua kali.

Hata hivyo, wapo watu wanaopenda kuwa na kipara kutokana na sababu mbalimbali lakini hushindwa kuwa na hicho cha asili. 
Ili kutekeleza kiu yao wao hunyoa upara kwa kumaliza nywele zote kichwani na hii imekuwa ikafanyika kwa vijana, wazee bila kujali jinsi. 

Mtaalamu wa magonjwa ya ngozi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Baraka Chaula anasema kuwa kwa hapa nchini hakuna utafiti juu ya kipara uliowahi kufanyika katika miaka ya nyuma. 
Labda iwe kwa miaka ya karibuni lakini katika miaka iliyopita, sijaona kumbukumbu yoyote ya utafiti wa kipara kufanyika,” anasema Dk Chaula. 

Pamoja na hali hiyo, anasema suala la kipara linaweza kuchukuliwa ni sehemu ya tatizo la ngozi kutokana na namna lilivyo, sehemu linapotokea pamoja na athari zake.

Wao kama wataalamu, anasema wanaamini tatizo la kipara linaweza kusuluhishwa iwapo chanzo chake kitagundulika mapema na hatua za kitiba kuchukuliwa. 
Anasema kipara kinachosababishwa na kaswende kinaweza kuzuilika iwapo tiba ya ugonjwa itafanyika kwa wakati. 

Kuhusu kuwakumba zaidi wanaume kuliko wanawake, Dk Chaula anasema kipara ni tatizo la homoni za kiume zaidi.“Hata wanawake hupata kipara lakini hili huwapata wanaume zaidi kwa sababu ni tatizo la homoni za kiume,” anasema Dk Chaula.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na,: 0787 032 458

Credit Mwananchi.

Thursday, July 24, 2014

Maajabu:Kijana mwenye umri wa miaka 17 ang'olewa meno 232, tizama video hapa

Madaktari nchini India wametumia saa 7 kufanikisha upasuaji wa kinywa cha kijana Ashik Gavai mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa akipata maumivu ndani ya kinywani .

Dr Sunanda Dhiware, mkuu wa Kitengo cha tiba ya meno katika hospitali ya JJ mjini Mumbai ameiambia BBC kuwa wamefanikiwa kuyang’oa meno 232 kinywani mwa Ashik aliyeletwa hospitalini hapo akiwa amevimba taya huku akilalamika kwa maumivu makali.

Madaktari wamesema wamelazimika kutumia nyundo na tindo kuyatoa meno hayo na wakadai kwamba hilo ni tukio la ajabu na linaingia katika rekodi ya dunia.Hata hivyo Upasuaji huo umehusisha jopo la madaktari wanne.

Dr Dhiware anasema katika uzoefu wake wa miaka 30 ya udaktari wa kinywa na meno hajawahi kukutana na tukio la namna hiyo. Ameongeza pia kuwa kulingana na vitabu vilivyopo vinasema hali kama hiyo inaweza kujitokeza katika taya la juu na meno yaliyowahi kung'olewa katika hali hiyo yalikuwa 37 lakini cha kushangaza ni kuwa tukio la Ashik Gavai limetokea katika taya ya chini na ameng'olewa meno 232 idadi ambayo ni kubwa huku akisalia na 28 kwa matumizi yake ya kawaida wakati kitaalamu mtu mzima anapaswa kuwa na meno 32.
Baba mzazi wa kijana Ashik ,Suresh Gavai amenukuliwa akisema mtoto wake alikuwa akilalamika kwa miezi kadhaa juu ya maumivu na kwamba walidhani inaweza kuwa ni matatizo ya saratani na ndipo wakamleta Mumbai.

Utafiti: Kulala zaidi ya masaa saba ni hatari sana kwa afya ya binadamu

Wakati ambapo tafiti za awali zilionesha kuwa kulala muda mrefu kunaweza kusaidia zaidi kuweka sawa afya zetu, tafiti mpya zimeonesha kuwa kulala zaidi ya masaa saba ni hatari sana kwa afya ya binadamu. 

Utafiti uliofanywa na Shawn Youngstedt, Professor wa chuo kikuu cha Arizona State umebaini kuwa kulala zaidi ya masaa saba au chini ya masaa saba ni hatari kwa mwili wa binadamu. 

Akiongea na Wall Street Journal, professor Shawn Youngstedt amesema kuwa alifanya utafiti kwa watu 9,000 na kubaini kuwa watu wenye umri kati ya miaka 50 hadi 64 waliolala chini ya masaa sita usiku au waliolala zaidi ya masaa nane wana matatizo ya kumbukumbu na uwezo mdogo wa kufanya maamuzi.

''The lowest mortality and morbidity is with seven hours,' says .But eight hours or more has consistently been shown to be hazardous,Just last month a study of almost 9,000 people found those aged 50 to 64 who slept for less than six hours a night - or more than eight - had worse memories and decision-making abilities.”  

Kwa hiyo tunashauriwa kulala kwa muda wa masaa saba tu usiku, sio chini ya hapo na sio zaidi ya hapo.

Wednesday, July 23, 2014

Utafiti mpya waonyesha uwezo mkubwa wa kuangamiza kirusi vya UKIMWI, kukiua na kumkinga binadamu

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple, Marekani wamegundua dawa ya kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambayo ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na zilizowahi kupatikana katika tafiti za awali duniani. 

Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa. 

Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari juzi mjini Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao wamegundua namna ya kukiondoa kirusi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua. 
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.

Dk Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa kupenya ndani ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake, ndani ya mfumo wa damu. 

Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).” 

ARV huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi mwathirika anapoacha kutumia dawa. 

Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU.

Kama imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani. 
Alisema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo likawa gumu. 

Inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema. 
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.

Lazima dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na utendaji wa mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi zinaposhindwa… Tusubiri tuone hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” alisema Majani.

Mkutano wa Ukimwi  

Ugunduzi huo umekuja wakati wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli za kukata tamaa kwenye mkutano wa Ukimwi unaomalizika kesho huko Melbourne, Australia. 

Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za utafiti za VVU wameweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio kwa sababu dawa zake zinapotumika, vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya.

Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili ili visiathirike na kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty ya Australia, Profesa Sharon Lewin. 

Dawa mpya inavyofanya kazi  

Dk Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa protini maalumu ambayo inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta nje. 
Baada ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga mwilini mwa binadamu bila tatizo.

VVU kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha kuzalishia virusi vingine. 
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU. 

Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk Khalili. 
Alisema tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama.

Katika maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100. 
Dk Khalili anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache...

Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu.”  Alisema wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya tiba ya binadamu. 

Kwa namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema wanaweza kuitumia kwa ajili ya kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa na hata kuwakinga wale ambao siyo waathirika.

Uzuri wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo kuingiliana kiutendaji. 
Ugunduzi wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa la Elimu ya Sayansi la National Academy of Science la Marekani na kuonekana kuvuta hisia za wengi. 

Hali ya Ukimwi duniani  

Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa Lewin alisema tafiti za sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 14 duniani wanaishi na VVU. 
Alisema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.

Alisema ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha matumaini waliotarajia ya kupata kinga na chanjo, bado juhudi zinaendelea ili kuhakikisha wanafikia mahali HIV inakuwa haina nafasi katika mwili wa mwanadamu. 
Alisema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, bado anaamini kwamba ipo siku chanjo na tiba vitapatikana. 

Wanasayansi waliohudhuria mkutano huo waliitaka dunia isiogope kutokana na kushindwa kwa baadhi ya tafiti kama ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la Mississippi, nchini Marekani ambaye alitangazwa amepona na baadaye virusi vikaibuka upya.

Credit Mwananchi.

Tahadhari Facebook: Kubofya video ya msichana anaevua nguo zote itasaidia hackers kuteka akaunti yako

Tafiti zinaonesha kuna idadi kubwa ya watu wanaotumia Facebook hubofya zaidi picha au video zinazoonesha matukio yanayoendana na ngono ama picha chafu. Lakini imebainika kuwa baadhi ya video hizo hutumiwa na hackers kuweza kuaccess taarifa za mtumiaji na kuteka akaunti yake. 

Wataalamu wa masuala ya mitandao wa Uingereza wamewatahadharisha watumiaji wa Facebook na kuwataka kuwa makini na video zinazosambaa zikionesha msichana au mwanamke (hata kama wanamfahamu) akiwa anavua nguo na kuonesha kuwa ukibofya itakupeleka Youtube kuangalia video nzima. 

Wameeleza kuwa video hizo hutuma taarifa zisizotegemewa kwenye browsers kwenda kwenye flash player na kisha kuiba taarifa za siri za mtumiaji.

Cadaver: Maiti zinazotumiwa na wanafunzi wa sayansi ya tiba

Mwaka 335-280 nchini Ugiriki kabla ya kuzaliwa kwa Kristo alitokea mwanasayansi nchini humo aitwaye Herophilus, huyu ndiye mtu wa kwanza kujenga mafunzo juu ya maumbile ya mwanadamu, kitaalamu ‘Anatomy’.

Mwanasayansi huyu ndiye baba wa somo la Anatomy yaani maumbile ya mwili. Huyu ndiye aliyebainisha kuwa ndani ya mwili wa mwanadamu kuna damu na si hewa.

Kwa kutumia taaluma hiyo alianza kujifunza kufanya upasuaji wa maiti ili kujifunza na kuzifahamu sehemu zinazounda mwili, ikiwamo ngozi, mishipa ya damu, ya fahamu, misuli na ogani za mwilini.

Kutokana na mafanikio yake na umuhimu wake kuelekea katika fani ya tiba, somo la upasuaji wa maiti ulianza kutumika duniani katika vyuo vya tiba.

Ingawa palitokea upinzani wa kidini wakitaka jambo hili lizuiliwe, paliwekwa taratibu maalumu zilizokubalika na kusimamiwa kisheria.

Upasuaji maiti  

Wanafunzi wote wanaosoma sayansi ya tiba duniani mwaka wa kwanza hufanya upasuaji wa maiti ili kujifunza maumbile ya mwanadamu yalivyo, hii husaidia katika fani ya utabibu kwani maiti hizo zinakuwa ndiyo mgonjwa wa kwanza wa mwanachuo.

Mwaka 1831, ilihalalishwa kisheria kwamba miili iliyokosa ndugu au kutotambulika, itumike kwa wanafunzi wa chuo wanaosomea fani ya sayansi ya tiba.
Kwa bahati mbaya hapo baadaye ikaonekana maiti za namna hiyo si rahisi kuzipata huku mahitaji yakiongezeka.

Mwaka 1839 huko Chicago, Marekani ulianzishwa utaratibu maalumu wa kuomba watu kujitolea miili yao pale watakapofariki ili itumike kwa ajili ya kujifunzia maumbile ya mwanadamu. Zikawekwa kanuni na sheria kuhusu muundo mzima wa jambo hilo bila malipo. Taratibu hizo zilirithiwa sehemu mbalimbali duniani lakini hufanyika kwa usiri mkubwa.

Cadaver ni nini?  

Ni maiti za watu ambazo hutumiwa na wanafunzi wa vyuo vya tiba kwa ajili ya wanafunzi kujifunza na kuona maumbile ya mwili mzima.

Maiti hizi zinaweza kuwa ni zile ambazo zimekosa ndugu au kutambuliwa au hakuna anayezitafuta au za watu waliojitolea kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria.

Wanafunzi huanza kujifunza kupasua kuanzia kichwani mpaka miguuni. Sehemu ya ngozi ambayo ni ya kwanza huanza kutenganishwa na huchunwa vizuri ili kuwezesha kuona sehemu za ndani za mwili kama mishipa ya damu, fahamu na misuli.
Hii ndiyo sababu ya ngozi ya maiti hizi kukutwa zimechunwa ili kuona vizuri maumbile ya ndani.

Jinsi zinavyotunzwa  

Ikishathibitika kwamba hakuna mtu aliyekwenda kuomba maiti husika kwa kipindi cha miezi 6-12, miili hiyo hukabidhiwa kwa wataalamu wa afya ambao huiwekea dawa maalumu iitwayo 2-phenoxethanol au fomalini.

Dawa hiyo huingizwa katika mshipa mkubwa wa paja na kisha kuieneza sehemu yote ya mwili kupitia mfumo wa mishipa ya damu ili isioze kwa miaka mingi. Hakuna mdudu au mnyama anayeweza kuila au kuigusa, ndiyo maana huendelea kukauka.

Dawa hii ni kemikali zinazoweza kusababisha saratani mwilini kama mtu atakuwa akikumbana nayo kwa muda mrefu na ina harufu kali inayokereketa, pia ni rahisi kuwa kama mvuke ambao mtu akivuta hupata shida kupumua.

Kuhifadhi, matumizi  

Baada ya kuandaliwa, viungo hivi huhifadhiwa katika vyombo au beseni maalumu lililojaa dawa ya maji ya fomalini mpaka pale vitakapohitajika.  Baada ya hapo nchi zilizo mbali hubadilishana maiti hizi. Kwa mfano, Tanzania ambayo iko Afrika Mashariki inaweza kubadilishana na nchi za Afrika Magharibi.
Jambo hili hufanyika kwa umakini mkubwa, haijawahi kuripotiwa mtu aliyekwenda kusoma fani ya tiba akakuta ndugu au rafiki anayemjua akiwa ni cadaver.

Pia katika nchi nyingine, wanafunzi hupewa siku saba kuamua kuendelea na masomo au la, baada ya kutembezwa katika maabara hizi za cadaver na hapa ndipo safari ya kuwa mwanasayansi wa tiba inapoanzia.

Kwa kawaida wanafunzi wanne hutakiwa kutumia cadaver moja na pia hutakiwa kuziheshimu na kutotoa siri za maiti hizo.

Jinsi zinavyotupwa, kuharibiwa  

Maiti hizi baada ya matumizi, mabaki yake huwekwa katika mifuko maalumu na kufungwa vizuri na kurudishwa katika taasisi husika iliyo na mamlaka ya kuzigawa katika vyuo.
Taasisi hiyo ndiyo inayohusika kuzika mabaki hayo.  Baadhi ya nchi huamua kuziteketeza kwa moto na wengine huzizika kama maiti nyingine.

Credit Mwananchi.

Siri utupaji viungo vya maiti yabainika, IMTU yakiri kuhusika na jinsi ilivyo tokea utupaji

Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na sakata hilo. 
Makamu Mkuu wa Chuo cha International Medical and Technological University (IMTU), Profesa PV Prabhak Rao (mwenye koti la blue)  na viongozi wengine wakisindikizwa na polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam jana, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo vya binadamu eneo la Mpigi Bunju. Picha na Rafael Lubava 

Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya IMTU. 

Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu.

Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo. 

Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa ajili ya  kutupwa eneo la Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova. 

Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali.  “Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema. 

Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu. 
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). 

Alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kujua sheria gani imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo na kwa nini wasitumie utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna makosa ya kisheria, hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Muhimbili wapokea mabaki  

Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya binadamu na kuhifadhiwa wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni suala la polisi, ninachoweza kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.

IMTU yakiri kuhusika  

Wakati Kova akisema hayo, uongozi wa IMTU ulikiri kuhusika na mabaki ya miili hiyo yaliyotupwa katika mto huo usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita. 
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dk Fariji Mtango alisema jana kwamba anaamini miili hiyo inaweza kuwa ni ile iliyotoka katika chuo hicho, ambayo imekuwa ikifanyiwa mazoezi na wanafunzi kwa kuwa walihitaji kuiteketeza na walishatoa agizo hilo. 

Alisema walitoa agizo kwamba mabaki hayo yapelekwe Muhimbili kwa mujibu wa utaratibu wao kwa kuwa hayakuwa na matumizi tena, kwa kuwa ndiyo sehemu yenye uwezo wa kuyateketeza na kutoa jukumu hilo kwa mmoja wa wakufunzi wa chuo hicho ambaye jana alikuwa safarini. 

Sasa zaidi hatujui kilichoendelea lakini tulipoangalia jana (Jumatatu) tulikuta sehemu yalipohifadhiwa imesafishwa, hivyo inawezekana ni sehemu ya vile vilivyoondolewa hapa. Hatukutarajia kwamba vingetupwa katika eneo lisilokuwa sahihi kama ilivyofanyika,” alisema.

Dk Mtango alisema hiyo ilikuwa moja ya hatua za kupisha wakaguzi ambao walitarajiwa kukuta maeneo yote ya kufundishia yakiwa katika hali ya usafi na unadhifu. 
Hawa wakaguzi wanapokuja wanatakiwa waone vitu vyote vikiwa sawa. Hata kama wangeona hayo mabaki ya miili ya binadamu isingekuwa tatizo, bahati nzuri wamekuja jana na wamefanya kazi yao vizuri,” alisema. 

Muda mfupi baada ya kutolewa kauli hiyo, viongozi tisa wa chuo hicho na walinzi wawili walikamatwa mnamo saa 7.30 mchana na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambako wanashikiliwa, lakini baadaye Kova alisema waliokamatwa ni wanane. 

Jana mchana eneo la chuo cha IMTU lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliotanda kuanzia getini, mapokezi na kwenye bustani za chuo hicho na wengine waliovalia sare maarufu kama ‘tigo’ ambao walikuwa wakishika doria mbele ya chuo hicho.

Hatua kuchukuliwa  Dk Mtango alisema uongozi wa chuo hicho umeshtushwa na kutupwa kwa mabaki hayo katika utaratibu usiokubalika na utafanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa wote waliohusika. 
Tunaanza na huyu ambaye tulimpa hili jukumu. Yeye ndiye aliyetakiwa kusimamia na anaujua wazi utaratibu wetu. Kwa sasa hajafika hapa na hata simu yake haipatikani. Tunaarifiwa kwamba amekwenda Zanzibar,” alisema.

Jinsi ilivyotokea  

Juzi jioni, ilitokea taharuki baada ya wananchi kubaini viungo hivyo na taarifa kuanza kusambaa katika mitandao ya kijamii na baadaye vyombo vya habari na hadi jana mjadala kuhusu suala hilo ulikuwa mzito na wananchi wakihoji miili hiyo ni ya watu gani, imetoka wapi na imetupwa na watu gani. 

Shuhuda wa tukio hilo, Mariam Nkumba alisema mara ya kwanza aliona mifuko yenye viungo hivyo Jumapili alipokwenda kuponda kokoto katika eneo hilo lakini hakubaini kulikuwa na nini. 

Siku hiyo, Nkumba alisema aliondoka katika eneo hilo saa 12 jioni bila kujua nini kilikuwa ndani ya mifuko hiyo na siku iliyofuata (Jumatatu), alikwenda kuchukua mfuko mmoja ili ahifadhie kokoto zake, ndipo aliposhtuka kuona viungo vya binadamu.

Mifuko ilikuwa mingi kweli, yote ilikuwa imejaa viungo vya binadamu. Mpaka sasa sijala na sina hamu ya kula. Ukiiona ile miili huwezi kula chakula,” alisema. 
Mfanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Skol iliyopo karibu na eneo hilo, Supery Kaijunga alisema mara alipopata taarifa kutoka kwa Nkumba alianza kutoa taarifa kwa wananchi wengine ili kwa pamoja wajue la kufanya. 

Baadaye walitoa taarifa polisi ambao walifika saa mbili usiku na kukusanya mabaki yote na kuondoka nayo. 
Hata hivyo, Kaijunga alieleza wasiwasi wake kuhusu wingi wa miili hiyo na kuhoji walikuwa watu gani na walitoka maeneo gani. 

Tukio hili siyo la kawaida na halijawahi kutokea huku kwetu. Tunakuwa na wasiwasi sana labda nasi maisha yetu yatachukuliwa kama hawa; polisi wafanye uchunguzi wa kina kubaini ukweli wake,” alisema Kaijunga. 

Imeandikwa na Andrew Msechu, Peter Elias na Pamela Chilongola
Credit Mwananchi.

Monday, July 21, 2014

Baada ya kueleza juu ya Watanzania wanavyo tumikishwa kwenye madanguro ya China, ahojiwa na shirika la Polisi la Kimataifa

Dar es Salaam. Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol), Tawi la Tanzania, limemhoji kwa saa kumi na moja binti aliyerubuniwa na kupelekwa China ambako kwa miezi mitatu alikuwa akitumikishwa kwenye madanguro nchini humo. 

Siku chache zilizopita, gazeti hili liliandika mfululizo, makala kuhusu msichana Munira Mathias, (si jina lake halisi) aliyetumikishwa kwenye madanguro nchini China, baada ya kurubuniwa kwamba alikuwa akipelekwa kufanya kazi kwenye hoteli kubwa. 

Munira alisema baada ya taarifa zake kuandikwa na gazeti hili Interpol walimtaka afike ofisini kwao kwa mahojiano. Mara ya kwanza alihojiwa kwa saa saba na aliitwa tena mara ya pili na kuhojiwa kwa saa tatu na nusu. 
Walinihoji jinsi safari yangu ilivyokuwa na namna ambavyo wale wanawake waliotuchukua kutoka hapa (Tanzania) hadi China na walivyosuka mipango ya kunisafirisha,” alisema.

Alisema: “Walikuwa wanataka kuendelea kufahamu kwa kina jinsi nilivyosafirishwa na walionisafirisha, hata hivyo nimewapa ushirikiano wa kutosha.
 
Mkuu wa Interpol Tawi la Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri ofisi yake kumhoji Munira na kwamba lengo ni kufahamu kwa undani jinsi Watanzania wanavyotumikishwa kwenye madanguro hayo, pamoja na kujua jinsi biashara ya binadamu kati ya China na Tanzania inavyofanyika. 
Nia ilikuwa ni kujua namna wasichana wanavyotolewa hapa na kupelekwa huko, lakini kikubwa ni kufanya kazi yetu kukomesha biashara hiyo kimataifa,” alisema Babile. 

Alisema siyo mara ya kwanza kwa Interpol kufanya jitihada za kukomesha biashara ya binadamu na kwamba hatua zimekuwa zikichukuliwa kila mara na siyo kwa Watanzania pekee, bali hata raia wa kigeni wanaokuja nchini. 

Tunafanya hii operesheni mara kwa mara. Kwa mfano, waliwahi kuletwa wanawake kutoka Nepal, walipofika hapa hati zao za kusafiria zikafichwa na wale wanaowatumikisha na wakaanza kufanya biashara ya ukahaba na baadaye kuwalipa wale waliowaleta,”alisema Babile.

Alisema kitengo hicho kimewahi kuwarudisha wanawake kutoka China waliofika hapa nchini kwa nia ya kufanya biashara ya ukahaba. 
Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Lucy Ngonyani ambaye ndiye aliyemhoji Munira alisema wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio la binti huyo kupelekwa China na matukio mengine yenye uhusiano au kufanana na hilo. 

Atishiwa kifo

Wakati hayo yakiendelea, Munira amesema hatua yake ya kuweka wazi ukatili aliofanyiwa China umemfanya aishi kwa shaka baada ya kusikia kuwa wanawake wa Magomeni ambao anawataja kuhusika kumsafirisha wanamsaka ili kumdhuru. 

“Nilipata taarifa kutoka kwa rafiki yangu mmoja (jina linahifadhiwa) ambaye tulikuwa naye China, aliniambia wale mabosi wetu wa China wamewapa taarifa wanawake wa Magomeni ili wakinipata popote waniue,” alisema Munira. 

Alisema alianza kuona dalili hizo tangu alipotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akitoka China kwani walikuwapo baadhi ya wanawake ambao walishiriki katika mipango ya safari yake. 
Alisema aligundua kuwa mawakala waliomsafirisha wanamtafuta walipomfuata rafiki yake aliyemsindikiza na kuuliza ni wapi anakoishi hivi sasa.

“Hali hiyo inanitia shaka sana na ndiyo maana naishi maisha ya kujificha hata vyombo vya usafiri wa umma situmii,” alisema. 
Kutokana na tishio hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba amesema hicho kinaandaa taratibu za kumsaidia msichana huyo kisheria. 
“Tumeshazungumza naye, kwa bahati mbaya leo (jana) aliitwa mahali lakini ilikuwa aje hapa na tufanye mipango ya kumsaidia kisheria,” alisema Dk Bisimba. 

Alisema kituo hicho kinalaani biashara ya usafirishaji wa binadamu na kuwataka wasichana wote waliowahi kufanyiwa vitendo hivyo kuwa na ujasiri wa kusema ili sheria zichukuliwe dhidi ya wahusika. 
“Tulipambana mpaka sheria ya kudhibiti usafirishaji wa binadamu ikatungwa, awali iliwekwa pamoja na ile Sheria ya Makosa ya Kujamiiana lakini hivi sasa ni sheria inayojitegemea,” alisema.

Taasisi nyingine iliyojitokeza kumsadia binti hiyo ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), ambacho kimeahidi kukutana naye ili kuona jinsi ya kumsaidia. 
Munira alipelekwa China katika Jimbo la Guangzhou na kufanyishwa biashara ya ukahaba baada ya kurubuniwa kuwa anakwenda kufanya kazi katika hoteli kubwa. 
Pamoja na manyanyaso mengine, aliwahi kubakwa na wanaume wanne wa Nigeria na kuambukizwa magonjwa ya zinaa pamoja na kushika ujauzito ambao hata hivyo, ulitoka baadaye.

Pamoja na adha hizo, alikuwa akiwajibika kuwalipa mabosi wake Dola 200 za Marekani (Sh330,000) kila siku, kutokana na fedha azizokuwa akipata kwa kufanya ukahaba.

Credit Mwananchi.

Friday, July 18, 2014

Wanakijiji Kusini Magharibi mwa Tanzania wanataka serikali ihalalisha matumizi ya 'Marijuana' Bangi

Huku harakati za kutaka matumizi ya Bangi kuhalalishwa zikishika kasi katika sehemu mbali mbali duniani, Tanzania haijaachwa nyuma.  
Wanakijiji katika wilaya ya Makete , mkoa wa Njombe Kusini Magharibi mwa Tanzania wanataka serikali iweke sheria ambayo itaweza kuhalalisha matumizi ya mmea huo.

Wanakijiji hao zamani walikuwa wakitumia mbegu za mmea huo kukaanga na chakula lakini siku hizi wanalazimika kuzitumia kwa usiri mkubwa wakihofia kukamatwa na polisi. 
Mwenyeketi wa Halmashauri ya wilaya ya Makete Daniel Okoka amesema matumizi ya Bangi katika wilaya hiyo hayajaanza leo, tangu zamani watu kitamaduni walikuwa wakitumia Mbegu za Bangi kukaanga na chakula. 
Na kama mmea huo ungekuwa na tahri kubwa kiafya, basi watu wengi wilayani humo wangekuwa vichaa.

Miti ya mimea hiyo pia ilikuwa ikitumiwa kutengeza kamba ambazo anasema zilikuwa za nguvu sana. 
Lakini kwa sababu ya sheria kali, matumizi ya Bangi au Marijuana yanafanywa kichinichini katika wilaya hiyo. 
Mwandishi wa BBC Leonard Mubali, anaandaa taarifa hiyo huko wilayani Makete na baadaye utaweza kuisikiliza katika redio na hapa kwenye mtandao. 

Lakini kwa sasa tunaulijza je ni ni sawa kwa Bangi kuhalalishwa kama chakula nchini Tanzania? toa maoni yako kwenye blog hii hapo chini kwakutumia facebook.

Thursday, July 17, 2014

'Nimeua, Nimekula nyama za Watu' Mtoto wa miaka 12 asimulia jinsi alivyofundishwa Uchawi

MTOTO mmoja mkazi wa Kimara Salanga, jijini Dar es Salaam (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 12 hivi karibuni aliibuka na kutoa madai mazito, akimtuhumu baba yake mkubwa kuwa alimfundisha uchawi, Ijumaa lina mkasa kamili.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, mtoto huyo alisema alianza kufundishwa tabia hiyo mbaya na baba yake mkubwa wakati huo akiwa na umri wa miaka mitano jijini Mbeya, kwa kumwelekeza namna ya kuroga na kuua watu. 

Katika mojawapo ya matukio makubwa aliyodai kuwahi kuyafanya ni pamoja na kutengeneza ajali ya boti iliyotokea Nungwi mapema mwaka huu ambapo yeye na wenzake walitumwa na baba yake huyo kutega mambo yao huku wengine wakipanda kwenye chombo hicho ili kuongeza uzito uliosababisha boti hiyo kuzama na kuua watu kibao. 

“Tuligandisha maji na kuweka sindano ambazo zilitoboa na baada ya watu kufa tulichukua nyama na damu kwa ajili ya kula na kunywa. Kwa hiyo nimeua na kula nyama za watu.

“Pia niliwahi kutumwa kwa msichana ambaye nilimnyunyizia dawa, nikamkalia na kumkaba shingoni mpaka akafa, nikamchukua na kumpeleka kwa baba mkubwa, pale kitandani niliacha gogo ambalo lina sura yake, kule tulimla na kunywa damu yake sisi na wachawi wenzetu. 

“Baada ya kufanya matukio hayo mazito, baadhi ya wananchi waliponigundua kuwa ni mchawi, walienda kunishtaki kwa mama yangu mzazi, wakimwambia asiponihamisha wataniua. 

“Kwa hali hiyo, huyu mjomba wangu akanileta Dar kwa ajili ya kufanyiwa maombi, lakini siku ya kwanza tu baada ya kufika, wakati nakwenda kuchota maji nilikutana na mmoja (jina limehifadhiwa) aliyeniambia kumbe mimi ni kijana wa kazi, alinitambua kutokana na nyota tunayobandikwa kwenye paji la uso baada ya kujiunga na uchawi ambayo ukikutana na mwenzako mnatambuana. 

“Baada ya kuniambia hivyo, usiku wake nikiwa nimelala, baba mkubwa alikuja kichawi na kunichukuwa na kunipeleka kwa yule mzee ambaye ndiye mkuu wa wachawi wa eneo hili, akanikabidhi kwake na mikoba yangu ya kichawi na hapo ndipo nikaendelea na kazi kwa upande wa huku Dar nikishirikiana na wachawi wengine.

“Kazi yetu mara nyingi ni kuloga, kuua na kunyunyizia dawa kwenye makaburi, yakifunguka tunachukuwa nyama za watu na mafuvu na kuyapeleka nyumbani kwa yule mkuu wa wachawi wa eneo hili tunapokutania. 

“Hapa nyumbani kwa mjomba niliweka dawa kwenye ukingo wa nyumba ili wasimalizie kujenga na kumloga mkewe ambaye tulimtupia vidonda vya tumbo, nilitaka kumuua lakini maombi yalimsaidia,” anasimulia kijana huyo.

Kwa mujibu wa shangazi yake aliyefahamika kwa jina la Lucy, baada ya kufanyiwa maombi kanisani kwa Mwingira, mtoto huyo alikiri kuachana na uchawi lakini alikuja kugundua bado anaendelea kutokana na kufanya maombi ya kufunga ambapo aliona katika maono kuna dawa ameweka kwenye nguo zake alizokuwa akipenda kuzivaa kila siku. 

Alipobanwa kwa vitisho ndipo aliwataja wachawi wenzake na kuongeza kuwa kila alipokuwa akitoka kwenye maombi, anakutana na wachawi wanamvisha uchawi tena na ule wa tumboni aliolishwa bado unaendelea kufanya kazi.

Baada ya kueleza mambo hayo mazito waliamua kutinga kwa mjumbe ambaye baada ya kuwasikiliza aliitisha kikao cha pamoja na yule mzee ambapo mtoto huyo alieleza kinagaubaga mbele ya wananchi mambo wanayofanya wakiwa na mzee huyo lakini alikataa na kuapa kwa kutumia msahafu kuwa anasingiziwa na kwamba hajawahi kufanya mambo hayo.

Mapaparazi wetu walitinga nyumbani kwa mzee huyo ili azungumzie suala hilo lakini jitihada ziligonga mwamba baada ya kumkosa ambapo mkewe anayedaiwa  kushirikiana naye kwenye mambo hayo, aliyejitambulisha kama mama Isha, alisema; 

“Ni kweli huyo mtoto alieleza mambo hayo kwa mjumbe lakini naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, mimi na mume wangu siyo wachawi, hayo ni maneno ya uzushi tu, watu wa kijiji hiki wanatuonea wivu kwa sababu tuna maendeleo kwani hawapendi mtu awe na mafanikio,” alisema.

Credit GPL.

Wednesday, July 16, 2014

Apania kuanzisha nchi ya kifalme Afrika, kutimiza amri ya bintiye

Mwanamme mmoja kutoka Marekani amedai umiliki wa kipande kidogo cha ardhi barani Afrika kama ufalme wake kwa sababu bintiye anataka kuwa binti mfalme  

Jeremy Heaton aliambia BBC kuwa amesafiri kutoka Virginia nchini Marekani na bendera yake kutangaza eneo hilo kwa Ufalme wa ‘Sudan Kaskazini’,  eneo hilo ni jangwa la mraba wa maili 800 lililo kati ya Misri na Sudan, na halijamilikiwa na nchi yoyote Alisema kuwa ameandikisha rasmi maombi kwa nchi hizo mbili, japo bado hajapata  jibu

Princess Emily akiwa amevaa tiara
‘Princess Emily’ huvalia tiara kila mahali anapokwenda kuashiria kuwa yeye ni mwanamfalme , bwana Heaton aliarifu BBC kuwa bintiye, Emily, aliuliza kwa sauti isiyo ya mzaha iwapo siku moja angekuwa binti mfalme ‘Kama babake, nilitambua kuwa ombi lake halikuwa mzaha, Heaton alisema. Nilitafiti vipande vya ardhi visivyomilikiwa na nikabahatika kuvigundua.’   

Ili kuadhimisha miaka saba tangu kuzaliwa kwa bintiye, Heaton alisafiri kwenda panapofahamika na wenyeji kama ‘Bir Tawil’ ili kutimiza ombi la Emily

Picha  ikionyesha kipande cha ardhi cha Bir Tawil  kinachotakiwa na Bwana Jeremy Heaton ili aweze kukitawala kama mfalme wa eneo hilo
Heaton ambaye ana watoto watatu alisema kuwa angefanya lolote ili kudhibitishia wanawe kuwa anaweza kuenda kokote kwa ajili yao ambapo tarehe 16, mwezi Juni, Heaton aliwasili jangwani na kuweka bendera iliyochorwa na bintiye, na kusisitiza madai yake ni halali       

Alidai kuwa kwa miaka mingi nchi kadhaa, ikiwemo Marekani, zilidai umiliki wa ardhi kwa kuweka bendera kwenye ardhi hiyo. Sasa bwana Heaton anasema atajaribu kuomba usaidizi kutoka kwa Umoja wa Afrika (AU)   

Mzozo wa mipaka kati ya nchi ya Sudan na Misri unaashiria kuwa jangwa hilo ni kati ya vipande vya mwisho duniani visivyomilikiwa,  tofauti, anavyosema, ni kuwa aghalabu vita huzuka ili kupata umiliki huo, bali kwa kesi yake, kuanzisha nchi hiyo ni ishara ya mapenzi yake kwa bintiye      

Hata kama hakuna uwezekano kuwa Jeremy Heaton atakuwa mfalme wa nchi hiyo mpya ya Sudan kaskazini, ana mipango atakavyoendeleza nchi hiyo

Binti mfalme Emily, aitwavyo sasa na familia yake, ametoa amri ardhi yake mpya iwe kituo cha ukulima. Sasa anavalia nguo za kimalkia na taji yake ya kifalme popote aendapo na anasema ‘inampendeza’ kuwa binti wa mfalme, lakini bado hajafahamu ni lini atakapozuru anachofikiria kuwa nchi mpya zaidi ulimwenguni

Itabidi Misri, Sudan na Umoja wa Mataifa kutambua ‘Ufalme wa Sudan’ kabla hajakuwa rasmi bintiye mfalme.

Tuesday, July 15, 2014

Je wagonjwa mahututi wasaidiwe kufa?

Askofu mstaafu wa Afrika Kusini Desmond tutu amesema kwamba anaunga mkono wagonjwa mahututi wanaotaka kusaidiwa kufariki wafanyiwe hivyo. 
Akiandika katika jarida la 'The Observer'',alisema yeye anasheshimu utu lakini hali inaweza kubadilika.

Pia alisema kuwa kuendeleza maisha ya Nelson Mandela ilikuwa kumvunjia heshima. 
Maoni ya askofu huyo mstaafu wa kanisa la kianglikana, ni sawa na yale aliyetamka Askofu mkuu wa kanisa la 'Canterbury Lord Carey' ambaye pia aliunga mkono usemi huo. 
Kanisa la kianglikana limeagiza uchunguzi kuhusu jambo hili.

Akiandika katika jadrida hilo, askofu huyu mstaafu wa kanisa la Anglikana Afrikakusini na mwenye miaka themanini na mbili alisema kwamba ''iwapo twahitaji mashine za kupumua,bila shaka tunahitaji kuuliza ubora wake na vile fedha zinavyotumika.'' 
Vile vile alieleza kuwa ni aibu vile aliyekuwa kiongozi wa Afrika Kusini Nelson Mandela aliwekwa hai kwa mda mrefu hospitalini katika hatua za mwisho za maisha yake huku akipigwa picha na wanasiasa waliomtembelea. 
Amesema kuwa Madiba hakujielewa kwa lolote na tendo lao lilikuwa ukiukaji wa heshima za hayati Mandela. 
'Ni kweli kwamba watu watahuzunika iwapo nitasema nisaidiwe kufa lakini kwa kauli yangu binafsi sina shaka na hilo.'' 
Tutu aliandika kuwa,hata ingawa amebadilisha maoni yake,uhakika wa hapo awali hautiliwi maanani kwenye uhalisia wa mambo yalivyo a hasa kwa wagonjwa walio mahututi.

Sheria kuhusu kusaidia wagonjwa mahututi kufariki nchini Uingereza?  

Kulinganaga na sheria ya Bunge ya 1961 inayohusiana na kujiua, ni hatia kuhamasisha au kufadhili mtu kujiua nchini Uingereza na Whales. Yeyote anayekiuka sheria hiyo huweza kufungwa gerezani hadi miaka 14. 
Sheria hii inakaribia kufanana ile iliyopo Kaskazini mwa Ireland.

Nchini Scotland kuna utata kwani hakuna sheria maalum inayohusishwa na kujiua, japo kwa maandishi na nadharia mtu huweza kuhukumiwa chini ya sheria zinazohusishwa na kujiua.

Je, Kumekuwepo na jaribio la kubadili sheria hiyo?  

Kumekuwa na majaribio kadhaa ya kuhalalisha ufadhili wa wanaotaka kusaidiwa kufariki ,lakini hakuna jitihada iliyofua dafu. 
Wanaharakati waliofanya majaribio ya kubadili sheria hiyo walibuni na kugharamia shughuli za tume itakayoshughulikia maswala yanayohusiana na ufadhili wa wanaotka kusaidia kufariki. 
Tume hiyo ilitoa kauli kuwa mnamo mwaka 2012 kulikuwa na kesi ngumu ya kuruhusu kufadhili kifo cha wagonjwa mahututi nchini Uingereza na Whales 
Hii ni kinuyume na madai yanayotolewa na taaluma ya matibabu, makundi ya kutetea haki za walemavu, na makundi mengine yanayodai kuwa sheria hiyo haifai kubadilishwa ili kulinda vikundi vilivyomo kwenye hatari ya kunyanyaswa na jamii.

Je, hali iko vipi ughaibuni?  

Katika nchi zingine kama Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi, sheria zimebuniwa zinazoruhusu kufadhili kifo.
Ufaransa inakadiria uwezekano wa kuanzisha sheria kama hiyo, japo kuna upinzani mkali kutoka kwa baraza la maadili ya matibabu nchini humo. 
Kundi la makampeni lifahamikalo kama "Dignity in Dying" linatabiri kuwa huenda nchi nyinginezo zikafuata mkondo huo wa kuhalalisha sheria hiyo. 
Hata hivyo askofu mkuu wa Canterbury, Justin Welby, anachukulia muswada huo unaohusiana na kufadhili kifo kuwa hatari na kanisa la Uingereza linataka swala hilo kupelelezwa. 
Kanisa hilo lilisema tume ya kifalme izingatie maoni ya kitaalamu na kukadiria kwa makini madai tofauti. Kanisa linaamini kuwa muswada uliopo sasa unafaa kutupiliwa mbali na kutoa nafasi ili upelelezi kufanywa. 
Watu 110 wanameandikishwa kuzungumza siku ya Ijumaa, muswada huo utakapojadiliwa. 
Askofu mkuu Desmond Tutu ametoa mwelekeo kuwa mjadala huo utafanyika siku ya kuadhimisha kifo cha Mandela, siku ambayo hayati Mandela angefikisha miaka 96.

Watoto wahamasishwe kushiriki michezo

Mwishoni mwa mwaka jana, uongozi uliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulifanya semina ya mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu au kushiriki katika michezo (grassroot) na baadaye tamasha kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Semina hiyo ilihusisha walimu wa mpira wa miguu kutoka sehemu mbalimbali nchini na tamasha liliwashirikisha watoto zaidi ya 1,500 wa Mkoa wa Dar es Salaam wenye umri kati ya miaka 6-12. 

Semina hiyo ilikuwa muhimu kwa sababu lengo lilikuwa ni walimu waliopata mafunzo, wakafundishe watoto wengi kupenda kushiriki katika michezo au kucheza mpira kwa furaha kwenye shule, mitaani ili kuwa na utamaduni wa Taifa la wapenda michezo kuanzia utotoni. 

Baada ya semina hiyo walimu walipewa vyeti vyenye nembo ya Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) kuonyesha wamehitimu mafunzo hayo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu au kushiriki michezo.

Pia katika tamasha lililofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, watoto walionekana kufurahia tamasha hilo kwani walifundishwa na walimu hao misingi mbalimbali ya soka. Watoto walioneka wakifurahia kukokota mpira, kupokea mpira, kutuliza, kupiga pasi na misingi mingine mingi. 

Sisi tunaamini walimu wale waliohitimu mafunzo hayo wanatumia vyema mafunzo waliyoyapata katika kuhamasisha watoto kushiriki katika michezo na hatutaamini kama walimu hao waliweka vyeti vyao majumbani kwao na kubaki kujisifu tu kwamba wamepata mafunzo ya Fifa. 

Tunaamini uongozi wa TFF uliopo madarakani hivi sasa na wenyewe utafanya semina nyingine ya mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu kwani huo ndiyo mwanzo wa kupata wanamichezo mahiri tangu ngazi ya chini.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia hivi sasa watoto wengi hasa wale wanaotoka katika familia zenye uwezo, wanaathiriwa na kuangalia sana televisheni na kucheza video games hivyo kuwa na wakati mgumu kiafya na kuwa imara kwa sababu hawafanyi michezo inayochangamsha mwili. 

Vile vile wale wanaotoka katika maisha duni wamejikuta wakifanya shughuli za kutafuta kipato ili kusaidia familia zao baada ya masomo badala ya kujishughulisha na michezo.

Tunaamini TFF inajua mtoto akishiriki katika michezo hukua vizuri, hujifunza nidhamu, hujifunza mambo ya msingi ya mchezo huo na hivyo inakuwa rahisi kwake kuendelezwa na zaidi ya yote anakuwa raia mzuri. 

Ikumbukwe kuwa michezo ni furaha, ni burudani, michezo huhusisha akili na mwili, kwa hiyo mtoto anayekua huku akishiriki michezo huusisha akili na mwili kwa kiwango cha juu. 

Tunaushauri viongozi wa vyama vya michezo waige mfano huo kwa kufanya semina za mafunzo ya walimu wa watoto na ikiwezekana kuandaa matamasha kama hayo ambayo hukutanisha watoto kutoka sehemu tofauti na kucheza kulingana na umri wao.

Pia vyama vifanye matamasha katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhamasisha watoto kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuwajengea mapenzi zaidi na michezo na hivyo kuandaliwa vyema kuwa watetezi wazuri wa taifa katika michezo hapo baadaye. 

Cheza mpira wa miguu kama lile lililofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwaka jana kwani yatasaidia kujenga msingi imara wa mchezo huo.