Select Menu

Ads

Random Posts

Powered by Blogger.

Design

Technology

Circle Gallery

Shooting

Racing

News

Bottom

Tuesday, August 5, 2014

Bibi ajitengenezea jeneza baada ya kuchoshwa na dhiki

Kila siku naomba Mwenyezi Mungu anichukue haraka ili nikapumzike kutokana na mateso ninayoyapata, lakini hofu yangu nikifa je, nitazikwa kama binadamu wengine? Ndiyo maana nimeamua kujitayarishia jeneza langu,” anasema Scholastica Mhagama (76) mwenye ulemavu wa viungo anayeishi pekee yake katika kibanda kilichoezekwa kwa nyasi. 

Bibi huyo mkazi wa Kijiji cha Lundusi Kata ya Peramiho wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, anasema kwa miaka mingi ameishi katika kibanda hicho alichojengewa na mzungu aliyemtaja kwa jina moja la Kilibada ambaye pia anasema alikuwa akimsaidia kulima mihogo. 

Anaongeza kuwa maisha yake yanategemea kukaa nje ya kibanda chake na kuomba msaada kwa watoto wanaopita ambao huwaomba wamchotee maji. 
Bibi Scholastica akiwa ameegemea jeneza lake.
 
Anabainisha kuwa mara chache anaweza kutokea mtoto ambaye humchotea maji kwenye ndoo ndogo ya lita kumi ambayo huyatumia kwa matumizi ya kuoga, kupikia, kunywa na kwamba hayatoshi kufulia wala kufanya kazi nyingine hali ambayo inamsababishia kuvaa nguo chafu wakati wote.

Anasimulia kuwa huwa anapika mara chache ndani ya kibanda anacholala na hata sehemu anayolala haina kitanda, godoro wala mkeka badala yake amekuwa analala chini katika mfuko wa mbolea na kujifunika blanketi kuu kuu. 

Ona kwanza mwanangu mahali ninapolala hakuna kitanda wala mkeka, mifuko ambayo ndiyo godoro langu huwa ninaomba tu. Nahitaji msaada, sina uwezo wa kufanya kazi yoyote tangu nilipokatwa mguu wa kulia nilipokuwa darasa la tatu hadi sasa nimekuwa naishi kwa shida ingawa sasa katika uzee hali imekuwa mbaya zaidi,’’ anasema. 

Ajitengenezea jeneza  

Kutokana na kushindwa kupata msaada kutoka kwa ndugu na majirani zake, Scholastica ameamua kutengeneza jeneza lake kabla ya kufa akihofia kuzikwa katika mkeka kwa kuwa ameshindwa kusaidiwa akiwa hai, hivyo anaamini akifa anaweza kutupwa kama mzoga wa mnyama asiye na faida yoyote.

Nimetengeneza kabisa jeneza langu siku nikifa wanizike humu. Naomba Mungu anichukue haraka ili kuepukana na mateso haya. Nimetengwa na jamii na majirani wanashindwa kunisaidia wanadai eti mimi ni mchawi kwa sababu watoto wangu wote wanne walikufa wakiwa wadogo. Naumia sana kusingiziwa kitu ambacho sikijui,’’ anasema kwa masikitiko. 

Bibi huyo anasema kuwa aliweza kutengeza jeneza hilo baada ya kupewa Sh40,000 na mfadhili mmoja. 

Tayari nilikuwa na mbao kwangu, hivyo kazi ilikuwa kumlipa kijana fedha na kumpa mbao ili anitengenezee jeneza,” anasema. 
Hata hivyo, aliitaja misaada ya haraka ambayo anahitaji ili aweze kuishi kuwa ni pamoja na baiskeli ya miguu mitatu (wheel chair) ambayo itamwezesha kutembea kwa kuwa hivi sasa amekuwa anatambaa na kupata maumivu makali kutokana na nyama iliyobakia kwenye nyonga baada ya kukatwa mguu.

Pia bibi huyo anahitaji msaada wa bati kwa ajili ya kuezeka kibanda chake kwa kuwa wakati wa masika mvua humnyeshea na kupata mateso makubwa. 

“Mvua yote inaishia mwilini mwangu. Huwa naugua na kupata homa kali lakini Mwenyezi Mungu bado hataki kunichukua. Napata vichomi kutokana na baridi kali hasa usiku hadi inanilazimu kuwasha moto kila siku usiku walau kupata joto. 
Kwa kweli natamani kufa lakini Mungu bado hajasikia kilio changu anataka niishi,’’ alisema kwa masikitiko. 

Alidai kuwa kuna watu walifika kumuandikisha jina na kumuingiza katika orodha ya watu wanaostahili kupata msaada na kwamba amekuwa anasikia misaada inafika kwa jina lake, lakini hajawahi kupewa hata shilingi.

Hajanywa chai kwa miaka 15  Akisimulia dhiki kuu aliyonayo bibi huyo anasema kwa siku walau anapata milo miwili, lakini chai hajawahi kunywa kwa miaka 15 sasa na kwamba kila siku anakula ugali kwa mboga ya majani aina ya ‘Chinese’ ambayo amekuwa anaomba na kupewa na wasamaria wema wanapopita njiani na kwamba katika kipindi cha miaka kumi sasa hajawahi kula nyama wala samaki. 

Anasema kulingana na matatizo aliyonayo ilitakiwa apelekwe katika kituo cha kulelea wazee wasiojiweza. Hata hivyo, Idara ya Ustawi wa Jamii imeshindwa kumsaidia kwa madai kuwa bibi huyo anaye kaka yake ambaye anamuelezea kuwa ni mzee asiye na uwezo wa kumlea. 

“Mwaka jana mwezi wa 10 nimelima hapa uwanjani matuta 12 kwa kushika jembe huku nimekaa chini na kujivuta, waulizeni majirani watawaambia ninahitaji msaada sina nguo, maji, sabuni, mafuta, pesa za matumizi mimi maisha yangu ni ya kuombaomba tu, alisema. 

Katika enzi za ujana wake wake Scholastica anasema alibarikiwa kupata watoto wanne ambayo wote walifariki wakiwa wadogo.

Hata hivyo kaka yake aitwaye Joackim Mhagama amekiri kuwa mwanzoni alipokuwa ana nguvu alijitahidi kumsaidia, lakini kutokana na umri kwenda ameshindwa kwani naye anahitaji msaada. 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lundusi chenye wakazi zaidi ya 2,500, Kelvin Mahundi amekiri kutambua matatizo aliyonayo Scholastica Mhagama na kwamba walimpeleka ustawi wa jamii ili kuhakikisha anapelekwa katika kituo cha serikali cha kulelea watu wasiojiweza. 

Anasema bibi huyo ilishauriwa apelekwe katika kituo cha Ngei wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma. Hata hivyo, hafahamu sababu zilizosababisha hadi sasa kutopelekwa katika kituo hicho ili aweze kusaidia hadi mwisho wa maisha yake.

Anasema hadi sasa kijiji hakina fungu la kusaidia watu wasiojiweza ingawa yeye kama mwenyekiti alipeleka taarifa zake kwa watu kama Abasia ya Peramiho ambao awali walikuwa wanatoa msaada pamoja na chama cha wenye ulemavu na kwamba inawezekana umri wake na ulemavu wake vinasababisha kushindwa kupata huduma muhimu. 

Kutokana na hali zao wanawake wazee wenye ulemavu kama ilivyo kwa Scholastica wanaishi katika maisha duni na ushiriki wao katika kazi za jamii ni mdogo kutokana na kukosa fursa na nyenzo za kuwasaidia kuleta maendeleo. 

Sera ya wazee  

Sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 inabainisha kuwa suala la uzee na kuzeeka limekuwa lenye umuhimu mkubwa ambapo karne ya ishirini imeshuhudia ongezeko kubwa la idadi ya wazee.

Kulingana na takwimu zilizopo, Tanzania inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 itaongezeka na kufikia milioni 8.3 (asilimia 10 ya watu wote). 

Hata hivyo, mwaka 2050, idadi ya wazee, kwa mara ya kwanza katika historia ya binadamu, inatarajia kuongezeka na kuzidi ile ya watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 24. Idadi hiyo katika Bara la Afrika pekee inatarajiwa kuongezeka kutoka milioni 38 ya sasa na kufikia milioni 51. 

Taarifa za Umoja wa Mataifa ya mwaka 1999 inaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya wazee duniani na kwamba ongezeko hilo linaonekana zaidi katika nchi zinazoendelea ambapo viwango vya ongezeko havilingani na uwezo wa rasilimali zilizopo za kuwahudumia wazee. 
Katika nyanja za afya, lishe na huduma nyingine za msingi kwa maisha ya binadamu.

Credit Mwananchi.