Washtakiwa hao ni pamoja na Jihad Swalehe, ambaye alisomewa mashtaka peke yake ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Watuhumiwa wa mtandao wa ugaidi nchini wakiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana walipofikishwa kusomewa mashtaka. Picha na Salim Shao
Washtakiwa hao ni pamoja na Jihad Swalehe, ambaye alisomewa mashtaka peke yake ya kula njama za kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo vya kigaidi.
Washtakiwa wengine ambao pia walisomewa mashtaka ya kula njama za kuingiza watu nchini na kushiriki vitendo vya ugaidi ni Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed na Mohamed Yusuph.
Wengine ni Abdallah Hassan, Hussein Ally, Juma Juma, Said Ally, Hamis Salum, Said Salum, Abubakari Mngodo, Salum Salum, Salum Amour, Alawi Amir, Rashid Nyange na Amir Juma.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mchana chini ya ulinzi mkali wa polisi na kisha walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo na jopo la mawakili wa serikali lililoongozwa na wakili mwandamizi, Prosper Mwangamila.
Mawaklili wengine ni George Barasa, Mwanaamina Kombakono na Brenda Nick. Kati ya waliopandishwa kizimbani, washtakiwa 16 ni wakazi wa Zanzibar na wengine wakazi wa Dar es Salaam.
Wakili Barasa alidai kuwa kati ya Januari, 2013 na Juni, 2014 katika maeneo tofauti nchini washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa kinyume cha Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002, kwa kuwaingiza watu ili wafanye makosa ya ugaidi.
Katika shtaka la pili, Barasa alidai kuwa katika kipindi hicho na maeneo tofauti nchini, kwa pamoja walikubaliana kuwaingiza Sadick Absaloum na Farah Omary ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Hellen Liwa anayesikilIza kesi hiyo aliwaeleza kuwa hawapaswi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa litasikilizwa na Mahakama Kuu.
Wakili Mwangamila alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba kesi hiyo itajwe tena mahakamani hapo Jumatano ijayo, akisema kuwa wanatarajia kuwa na maombi maalumu.
Hakimu Liwa alikubaliana na ombi hilo la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatano ijayo. Pia aliamuru washtakiwa kurudishwa rumande.
Baada ya washtakiwa hao kumaliza kusomewa mashtaka, alipandishwa kizimbani Swalehe na kusomewa mashtaka na wakili Brenda.
Wakili Brenda alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 21, 2013 na Juni 2, 2014, eneo lisilofahamika mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa alikula njama na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani, kutenda kosa la kusaidia kutenda vitendo vya ugaidi.
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa kwa kujua na kwa kutumia mawasiliano ya facebook aliwasiliana na Nero Saraiva na watu wengine kwa ajili ya kupata malighafi, fedha na ujuzi kwa nia ya kuweka mabomu sehemu tofauti nchini Kenya ili kusababisha majeraha na hofu kwa Wakenya.
Mshtakiwa huyo pia hakutakiwa kujibu chochote na upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi haujakamilika. Hivyo upande wa mashtaka uliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo..
Hakimu Liwa aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 31, 2014 itakapotajwa. Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mchana wakiwa ndani ya mabasi mawili yaliyokuwa yakisindikizwa na magari mawili ya Kikosi cha Kuzuia na Kutuliza Ghasia (FFU) na mengine watatu yaliyokuwa na askari wakiwa wamevalia kiraia.
Baada ya kusomewa mashtaka, washtakiwa waliondolewa mahakamani hapo kwa kutumia basi ndogo la magereza wakisindikizwa na magari manne ya FFU.
Credit Mwananchi.