Sambamba na hatua hiyo, Jeshi la Polisi limesema halitawaachia watuhumiwa wanane linaowashikilia hadi ukweli utakapojulikana.
Kamati hiyo imeundwa kuchunguza jinsi viungo hivyo vilivyotupwa, sheria zilizovunjwa na kupendekeza hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya wahusika wakiwamo viongozi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), ambao wamekiri kuwa viungo vilivyotupwa mara ya mwisho vilitoka katika taasisi yao.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Stephen Kebwe alisema jana kuwa kamati hiyo iliyoanza kazi juzi, inawashirikisha wadau muhimu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Hospitali ya Taifa Muhimbili na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
“Kwa sasa tunaendelea na kazi za kawaida kuratibu na kuhakikisha shughuli za kamati zinaendelea. Baada ya kamati kukamilisha kazi yake ndipo tutakapojua hatua za kuchukua na wanaostahili kuchukuliwa hatua,” alisema.
Kamati hiyo imeundwa wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilishatangaza kuunda jopo lake la uchunguzi, lakini alipoulizwa jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema kamati aliyounda ni sehemu ya hiyo iliyoundwa na wizara.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema kwa sasa hatarajii kama watuhumiwa hao wataachiwa hadi upelelezi na mahojiano yanayofanywa yatakapokamilika.
Kamanda Wambura alisema jalada linalowahusu watuhumiwa waliokamatwa Jumanne wiki hii, ambao ni viongozi wanane wa IMTU limehamishiwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Sakata lilivyoanza
Taarifa za kuonekana kwa viungo vya miili ya binadamu ikiwa imefungwa katika mifuko myeusi zilizagaa Dar es Salaam Jumatatu jioni huku wengi wakidai kwamba huenda kuna mauaji ya halaiki yaliyofanyika sehemu isiyojulikana.Baadaye Jumanne ilibainika kwamba viungo hivyo vya miili ya binadamu vilitupwa kimakosa na havihusiani na mauaji yoyote ya kukusudiwa, bali vilikuwa vikitumiwa na wanafunzi wa udaktari katika chuo cha IMTU kwa ajili ya mazoezi. Hata hivyo, viungo hivyo vilitupwa katika eneo hilo kinyume na taratibu zinavyoelekeza, hivyo viongozi wa chuo hicho kukamatwa na polisi.
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), juzi kilitoa taarifa kuhusiana na suala hilo kikiziomba mamlaka zinazohusika kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua.
Credit Mwananchi.